Na Kassian
Nyandindi,
Nyasa.
WANANCHI wanaoishi katika kijiji cha Nkalachi kata ya Liuli wilayani
Nyasa mkoa wa Ruvuma, wameiomba serikali na wadau mbalimbali wasaidie vifaa vya
kiwandani ili waweze kukamilisha ujenzi wa jengo la Zahanati ya kijiji hicho na
hatimaye waondokane na kero ya kukosa huduma za matibabu.
Aidha walisema kuwa hivi sasa akina mama wajawazito na watoto
wadogo wamekuwa wakifariki dunia, hasa pale wanapokuwa njiani kuelekea
Hospitali ya Anglikana iliyopo wilayani humo, ambayo ipo mbali nao kwa ajili ya
kutafuta matibabu.
Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wakazi wa kijiji hicho,
mbele ya Kamanda wa Umoja wa vijana wa chama cha mapinduzi (UVCCM), Cassian
Njowoka walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.
“Sisi wananchi tumeanza kazi ya ujenzi wa jengo la zahanati
yetu ya kijiji, tunawaomba wadau mbalimbali watusaidie kutoa mchango wao wa
vifaa vya kiwandani ili tuweze kukamilisha ujenzi wa jengo hili, akina mama
wengi wajawazito wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na kukosa
huduma za kitabibu”, walisema.
Kwa upande wake Kamanda UVCCM wilaya ya Nyasa, Njowoka baada
ya kusikiliza kilio hicho cha wakazi wa kijiji cha Nkalachi aliweza kutoa ahadi
ya kuchangia vifaa hivyo vya kiwandani, ikiwemo bati, nondo, mifuko ya saruji,
vitanda vya kujifungulia akina mama wajawazito pamoja na gharama za kulipa
mafundi ambao wanaendelea na kazi hiyo ya ujenzi.
“Ndugu zangu nitachangia vifaa vyote vya kiwandani mpaka
jengo hili litakapofikia hatua ya kukamilika ujenzi wake, naiomba kamati husika
ya ujenzi iketi chini na kufanya tathimini juu ya gharama hizi za ujenzi na
baadaye mniletee niweze kukamilisha”, alisema Njowoka.
No comments:
Post a Comment