Na Steven Augustino,
Tunduru.
MFUGAJI mwenye asili ya Mmang’ati, ambaye ametambuliwa kwa
jina la Alex Poketi (22) amelazwa katika Hospitali ya wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, baada ya kujeruhiwa vibaya na simba wakati akiwa machungani.
Walioshuhudia tukio hilo, walisema kuwa majeruhi huyo alipatwa
na mkasa huo wakati akijitosa kuokoa maisha ya ng’ombe wake ambao walivamiwa na
mnyama huyo mkali, kwa lengo la kutaka kuwafanya kitoweo.
Walisema tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Mbuyuni
kilichopo kando kando ya mto Ruvuma, eneo ambalo wafugaji hao wamekuwa
wakichungia mifugo yao tangu mwaka 2007.
Katika eneo hilo imeelezwa kuwa, simba huyo alijitokeza
ghafla na kuanza kushambulia ng’ombe hao aliokuwa akiwachunga ambapo Alex
alijawa na jazba na kwenda kumrukia simba huyo kwa kumchoma mkuki, jambo ambalo
lilimfanya mnyama huyo akimbie.
Wakati hilo likifanyika, ghafla simba huyo alijitokeza tena kwa
mara ya pili na kuanza kumshambulia kijana huyo kwa kumkwaruza na kucha zake
sehemu mbalimbali za mwili wake, hali ambayo ilimsababishia majeraha makubwa.
Mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta
Mmari Zabron alikiri kumpokea majeruhi huyo na kuongeza kuwa wamefanya jitihada
ya kumpatia matibabu kwa kumshona nyuzi, sehemu ambazo zina majeraha makubwa.
Alifafanua kuwa majeruhi huyo ana hali mbaya kwani bado
hajitambui kutokana na kuumizwa vibaya sehemu ya kifuani, mikononi na katika
mapaja ya miguu yake.
Japhet Mnyagala ambaye ni ofisa ardhi na maliasili wilayani
humo, alisema tayari amekwisha tuma kikosi cha askari wenye silaha kwa ajili ya
kwenda kumsaka simba huyo kwa lengo la kumuua, ili asiweze kuleta madhara
mengine makubwa kwa wananchi hapo baadaye.
No comments:
Post a Comment