Na Muhidin Amri,
Songea.
NAIBU Waziri wa mawasiliano sayansi na teknolojia January Makamba, amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kujenga barabara za mkoa wa Ruvuma, kwa kiwango cha lami hatua ambayo imewezesha kuharakisha shughuli za kiuchumi na maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo.
Barabara hiyo ni ile ya kutoka Songea hadi Mbinga yenye kilometa 96, Songea kwenda Namtumbo kilometa 76 na barabara ya Namtumbo hadi Tunduru yenye zaidi ya kilometa 220 ambayo ujenzi wake unaendelea.
Makamba ametoa pongezi hizo jana wakati alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani humo, baada ya kukamilisha zoezi la kutafuta wadhamini katika jitihada zake za kuomba ridhaa ya chama hicho, kumsimamisha ili aweze kupeperusha bendera ya kugombea Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ambapo wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini mgombea huyo.
Makamba sasa ni mgombea wa tatu sasa kwa nafasi ya urais kupitia Chama Cha Mapinduzi kufika mkoani
Ruvuma, kuomba udhamini akitanguliwa na wagombea wengine ambao ni Makongoro
Nyerere na Waziri wa Mambo ya nchi za nje, Bernard Membe.
Makamba alisema kuwa kazi
aliyoifanya Rais Kikwete ya kujenga barabara za mkoa huo kwa kiwango cha lami,
ni jambo la kupongezwa hasa ikizingatia kuwa mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa
michache hapa nchini, inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula ambapo aliahidi
kama atapata nafasi ya urais ataendeleza mambo mazuri aliyoacha Rais Kikwete, wakati
wa utawala wake.
Aidha alifafanua kuwa endapo
atachaguliwa katika uchaguzi mkuu ujao na kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha
anajenga Reli kutoka Mtwara hadi Mbamba bay na mji wa Songea kuufanya ndiyo kituo kikubwa cha reli hiyo,
kutokana na umuhimu wake kiuchumi.
Kwa mujibu wa mgombea
huyo wa chama hicho tawala, alieleza kuwa wakazi wa Ruvuma wamekuwa wakifanya
vizuri katika uzalishaji wa mazao mbalimbali ya chakula na biashara hata hivyo
ni jambo la kusikitisha kuona kiasi kikubwa cha mazao hayo, bado
yanaozea shambani au majumbani kwani hakuna soko la uhakika kwa wakulima hao.
Ameahidi kama
atabahatika kupata ridhaa ya wananchi kuingia Ikulu basi atajitahidi kuweka
mfumo mzuri ambao utamwezesha mkulima anapopeleka mazao yake sokoni, analipwa
fedha yake badala ya kukopwa jambo hilo limekuwa likiwaumiza wakulima na kusababisha
kuwa masikini.
Aidha amewataka wagombea
wengine katika nafasi hiyo kufanya kampeni zao kistaarabu na kuacha tabia ya
kuwachafua wengine, kwa sababu kufanya hivyo ni kukichafua CCM kwa kuwa hata
yule atakayechaguliwa bado ataonekana ana mapungufu makubwa na hana sifa ya
kuwaongoza watanzania.
“Kama kuna jambo
linaloniuma ndani ya chama chetu wakati huu wa kutafuta wadhamini ni tabia ya
baadhi ya wagombea wenzangu kuchafuana hali hii haileti picha nzuri, mwisho wa
siku atapatikana mgombea mmoja ambaye ni lazima wote tutamuunga mkono”, alisema
Makamba.
Alisema kati ya wagombea wote waliojitokeza na kuchukua fomu ya kutaka urais kupitia tiketi ya Chama cha mapinduzi ni yeye tu ndiye mwenye sifa ya kuwaongoza watanzania kwani amezaliwa, kukua, kulelewa na kufanya kazi ndani ya chama hicho kwa hiyo ana uzoefu mkubwa katika kuwatumikia wananchi.
Kadhalika aliongeza kuwa
Watanzania ni lazima waelewe kwamba hivi sasa nchi inahitaji mabadiliko ya
uongozi utakaokuwa tayari, kukabiliana na changamoto mbalimbali
ndani na nje ya chama na kamwe wasikubali kurubuniwa na watu wanaotaka uongozi
kwa kutumia nguvu kubwa ya fedha au kuwakashifu wenzao.
No comments:
Post a Comment