Baadhi ya Wataalamu kutoka katika kata mbalimbali wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wakiwa katika semina ya mpango wa TASAF kwa ajili ya kwenda kutoa elimu kwa wananchi vijijini. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
WANANCHI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameombwa kutoa
ushirikiano wa kutosha juu ya hatua zote zinazotakiwa kutekelezwa pale
unapofanyika upembuzi yakinifu katika matatizo yao, hasa yale yanayolenga uhifadhi
wa udongo, uvunaji maji, udhibiti makorongo na kuotesha vitalu vya miti.
Aidha wametakiwa kuondokana na dhana potofu ambazo zinaenezwa
na watu wasio na nia njema, kwa yale yanayofanywa katika awamu ya tatu ya
utekelezaji wa mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wakiwa na lengo la
kutaka kukwamisha maendeleo ya mpango huo, ili usiweze kuleta mafanikio katika
jamii wilayani humo.
Hayo yalisemwa na Peter Lwanda ambaye ni mmoja kati ya
watendaji wa mfuko huo, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi mtendaji wa TASAF hapa
nchini, Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo ya kuutambulisha juu ya kutoa ajira za
muda, kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini kwenye kikao cha kazi
kilichofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu tarafa ya mlingoti mjini hapa.
Lwanda alifafanua kuwa mpango huo, unafuatia uzinduzi uliofanywa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete Agosti 15 mwaka 2012
na kuanza kutekelezwa mwaka 2013 ukilenga kunusuru kaya maskini kwa kuziwezesha
kupata huduma muhimu hasa katika nyanja ya elimu, afya na maji.
Alisema mpango huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka kumi,
na kwamba kaya milioni moja zinazoishi hapa nchini, katika mazingira duni ya
umaskini zitafikiwa na kuwezeshwa.
Mpango huo wenye sehemu kuu tano, ikiwemo ya uhawilishaji
fedha kwa kutoa ruzuku katika kaya hizo ambazo zina watu wenye uwezo wa kufanya
kazi, kujenga na kuboresha miundombinu inayolenga katika sekta husika na
kujenga uwezo katika ngazi zote za utekelezaji.
Kadhalika mpango huo unatekelezwa na serikali pamoja na wadau
mbalimbali wa maendeleo, wanaochangia wakiwemo Benki ya dunia, Shirika la
Maendeleo la kimataifa la Sweeden (SIDA), Mpango wa maendeleo ya umoja wa
mataifa (UNDP), Shirika la umoja wa mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) pamoja
na Shirika la kazi la umoja wa mataifa (ILO).
Naye Fadhil Mshamu ambaye alikuwa akimwakilisha Mwenyekiti wa
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Faridu Khamis TASAF katika mpango huo wa awamu
ya tatu pia alieleza kuwa unalenga kaya maskini zenye watoto chini ya miaka
kumi na akina mama wajawazito waweze kupata lishe bora, huduma za afya, elimu,
maji ikiwemo na ajira kwa kupitia ruzuku za aina mbili, ya msingi na ya
kutimiza masharti maalumu.
Washiriki 48 kutoka kata mbalimbali wilayani humo, wamepatiwa
mafunzo juu ya utekelezaji wa mpango huo ambao walikuwa wakitoka katika makundi
ya wataalamu wa miundombinu ya maji, kilimo, umwagiliaji, afya, elimu,
mazingira na uvuvi ili baadaye huko waendako wakasaidie kuelimisha wananchi
katika maeneo yao juu ya utekelezaji wake.
No comments:
Post a Comment