Cresensia Kapinga. |
Na Mwandishi
wetu,
Songea.
CRESENSIA Kapinga (42) ambaye ni mwandishi wa habari, gazeti
la Majira mkoani Ruvuma ametangaza nia yake ya kugombea nafasi ya udiwani,
katika kata ya Ndilimalitembo Manispaa ya Songea mkoani humo, kupitia tiketi ya
Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kapinga ameweka vipaumbele vyake endapo wananchi wa kata hiyo
watampatia ridhaa ya kuwaongoza, kwamba atahakikisha huduma zifuatazo
zinaboreshwa kwa wananchi wake ambavyo ni elimu, afya, maji na miundombinu
mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Songea, Kapinga
alieleza kuwa dhamira ya kugombea katika kata hiyo alikuwa nayo tokea muda
mrefu, ambapo katika uchaguzi mkuu uliyopita mwaka 2010 aliwahi kugombea nafasi
hiyo kupitia viti maalum, lakini kura hazikutosha na sasa amerudi tena.
Alisema anaamini kwamba atashinda kwa kishindo kutokana na
vijana na wazee wa kata hiy,o kumpatia baraka kuwa wanamuhitaji agombee kwenye
kata ili aweze kuwaletea mabadiliko.
Alifafanua kuwa sababu kubwa iliyomsukuma kugombea nafasi
hiyo, ilitokana na maombi ya wananchi wa kata ya Ndilimalitembo ambao kwa muda
mrefu wamechoshwa na viongozi waliokuwepo madarakani kutoa ahadi ambazo
hawazitekelezi, licha ya ukweli kwamba kata hiyo ni moja kati ya sehemu ambayo
inawasomi wengi akiwemo Waziri wa nchi, Sera na Bunge Jenista Mhagama.
“Wananchi wameniomba nigombee katika nafasi hii, ili niweze
kuwa mwakilishi wao katika baraza la madiwani Manispaa ya Songea kwa kuwazungumzia
matatizo yao ya kimaendeleo ndani ya kata, ili niweze kusaidia kuyasukuma mbele
na mwisho wa siku waondokane na adha wanazoendelea kuteseka nazo”, alisema
Kapinga.
Alisema hivi sasa wananchi wa kata hiyo wanachohitaji ni kuona
mabadiliko makubwa ya kiuongozi ambayo wanaimani kufanya hivyo itasaidia
kuboresha maisha yao, kwa kile walichoeleza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona
licha ya wao kuwa wachapakazi lakini tokea kata hiyo ianzishwe hawajajengewa hata
zahanati au soko jambo ambalo lingewafanya wapige hatua.
Kukosekana kwa huduma hizo muhimu, kunasababisha wananchi hao
wateseke kwa kuzifuata umbali mrefu na endapo zingekuwa jirani nao wangeweza
kuondokana na kero hiyo.
No comments:
Post a Comment