Gari hili ndilo walilopata nalo ajali Wanafunzi na Padri wa kanisa katoliki jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WAUMINI wa madhehebu mbalimbali ya dini wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu cha
majonzi, kufuatia ajali ya gari lililoteketea kwa moto na kusababisha baadhi ya
wanafunzi na Padri wa kanisa katoliki wilayani humo, kufariki dunia.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki
Jimbo la Mbinga, John Ndimbo wakati alipokuwa akiongoza ibada ya mazishi ya
Padri Hyasint Kawonga ambaye alifariki dunia, kwenye ajali hiyo na kusababisha
vifo vya watu saba wakiwemo wanafunzi sita, Padri huyo na majeruhi 24.
Wanafunzi wanaosoma katika shule ya Kigonsera Catechists
Secondary School (KCS) iliyopo katika kata ya Kigonsera, akiwemo na Padri Kawonga
ambaye ni Mkurugenzi wa shule hiyo, Parokia ya Kigonsera katika jimbo hilo
walipoteza maisha baada ya gari walilokuwa wakisafiria, kutumbukia kwenye
korongo na kuteketea kwa moto.
Askofu Ndimbo alisema katika kipindi hiki cha majonzi na
maombolezo, kuna kila sababu ya waumini wa kikristo kuendelea kuwaombea marehemu
hao kwa kusali na kumuomba Mungu, azilaze roho zao mahali pema peponi.
Ibada hiyo ya mazishi ilihudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo
na viongozi wa dini kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, ambapo
mwili wa marehemu Kawonga umelazwa katika makaburi ya Parokia ya Kigonsera
wilayani Mbinga.
Kadhalika nao wanafunzi waliofariki ambao walikuwa wanasoma
katika shule hiyo ya KCS ambao ni Fidea Ndunguru(17) na Suzan Kawonga (17) wote
wa kidato cha nne miili yao ilisafirishwa kwenda katika kijiji cha Mpapa
wilayani Mbinga kwa ajili ya mazishi.
Wengine wawili walisafirishwa kwenda makwao ambao ni wa familia
moja walikuwa wakisoma kidato cha nne ni wa kutoka kijiji cha Namabengo wilaya
ya Namtumbo, ambao ni Gladness Ngonyani (17) na Kelvin Ngonyani (20) na kwamba
Damas Mbele (16) wa kidato cha pili kutoka kijiji cha Myanga yanga na Philoteus
Hyera (16) kijiji cha Mahenge ni wa kutoka wilayani Mbinga nao walisafirishwa
kwenda nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi.
Pamoja na mambo mengine, Kamati ya ulinzi na usalama wilayani
Mbinga, ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga
ilitoa masanduku saba ya kuzikia pamoja na gharama za usafiri.
Awali kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo
Msikhela alipozungumza na mwandishi wa habari hizi alifafanua kuwa ajali hiyo
ilitokea Juni 4 mwaka huu majira ya jioni, wakati Wanafunzi hao na Padri
Kawonga walipokuwa wakitoka shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa
ajili ya chakula cha wanafunzi shuleni hapo.
Padri Kawonga ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo ambalo
lilipata ajali lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya Land rover, One ten
baada ya kushindwa kupanda mlima katika eneo la Minazi kata ya Kigonsera ndipo
lilirudi nyuma na kutumbukia kwenye korongo kisha kuwaka moto huku ndani ya
gari, wakiwa wanafunzi na padri huyo ambao waliteketea kwa moto.
No comments:
Post a Comment