Na Steven
Augustino,
Tunduru.
TAARIFA potofu kuhusu utekelezaji wa mpango wa uhawilishaji
fedha ili kuziwezesha kaya maskini kujikimu kiuchumi, unaotekelezwa na Mfuko wa
Maendeleo ya Jamii (TASAF) awamu ya tatu wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, unadaiwa
kuendelea kuwa mwiba kwa wanufaika hali ambayo inawafanywa kushindwa kubuni
mikakati ya kujiendeleza, kupitia mfuko huo.
“Ingawa wataalamu wetu
wamekuwa wakitupatia elimu ya kujikwamua na umaskini kupitia vikundi vyetu vya
ujasiriamali, ambavyo tunawekeza katika vikundi vya Mpeano miongoni mwetu
wamekuwa wakiogopa kujiunga na vikundi hivi kutokana na kuhofia kuwa huenda
mpango huo, utakwisha kabla hawajamaliza mzunguko wa mpeano wao kwa sababu
chanzo ni uwepo wa taarifa potofu hivyo familia zao kukosa uwezeshaji huo”,
walisema.
Hayo na mengine mengi yalibainika kufuatia uchunguzi
uliofanywa na mwandishi wetu, wakati waratibu husika wa mpango huo wilayani
humo wakiwajibika kuelimisha wananchi wakati wa malipo ya fedha, kwa walengwa
waliokuwemo kwenye mpango huo katika vijiji vilivyomo wilayani humo.
Halima Chipala, Zaina Chipande na Fatu Chingulu kutoka kijiji
cha Mchoteka wilayani Tunduru, ni kati ya wanufaika waliotoa ukimya huo baada
ya kuwahoji wataalamu hao na kuongeza kuwa wengi wa wanufaika hao wamekuwa
wakipotoshwa na wananchi ambao hawapo kwenye mpango huo, kuwa endapo
wataanzisha vikundi hivyo vya mpeano ipo hatari miongoni mwao kutonufaika na
huduma husika.
Mbali na kuwepo kwa baadhi ya wanufaika wachache ambao
wamesema hivi sasa wameanza kujipanga kuunda vikundi vya uzalishaji mali,
ikiwemo kununua mifugo aina ya kuku, bata na mbuzi ili baadaye waifuge lakini
hali halisi ya utekelezaji inaonekana kuwa na changamoto nyingi zinazohitaji
walengwa, kupewa elimu ya kutosha ili kuondokana na tatizo hilo.
Wengi wa wanufaika wameonekana kuipongeza serikali, kwa
kubuni mpango huo ambapo wameonesha kuanza kuwekeza fedha walizopata ili hapo
baadaye ziweze kuwasaidia pale mradi utakapofikia kikomo.
Mzee Mustapha Tawakali na Khadija Mussa kutoka kijiji cha
Mkasale tarafa ya Namasakata wilayani humo, walisema kutokana na upotoshwaji
huo kuna kila sababu ya kuona kwamba wananchi inawafikia elimu ya kutosha
ipasavyo, ili hali hiyo isiweze kuendelea kuwepo miongoni mwa jamii.
Taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi mtendaji wa TASAF,
Ladislaus Mwamanga alisema mpango huo ulizinduliwa na Rais Jakaya Kikwete
Agosti 15 mwaka 2012 na kuanza kutekelezwa Februari 2013 unalenga kunusuru kaya
maskini, kwa kuzisaidia fedha ili ziweze kupata huduma mbalimbali ikiwemo katika
sekta ya elimu, afya na maji.
Kupitia mpango huo ambao utekelezaji wake ni wa miaka kumi,
utazinufaisha kaya milioni moja zinazoishi katika mazingira duni ya umaskini
zitafikiwa na kuwezeshwa kupitia mgawanyo wa sehemu kuu tano, ikiwemo ya
uhawilishaji fedha kwa kutoa ruzuku kwa kaya maskini zenye watu wenye uwezo wa
kufanya kazi kujenga na kuboresha miundombinu husika inayolenga katika sekta
hizo.
Taarifa hiyo inafafanua kuwa mpango huo utawezesha pia kaya
zenye watoto chini ya miaka mitano na akina mama wajawzito, ikilenga kuwapatia
lishe bora, huduma za afya, elimu, maji na ajira kupitia ruzuku za aina mbili
ya msingi na ya kutimiza masharti maalum.
No comments:
Post a Comment