Na Steven Augustino,
Tunduru.
KIKUNDI cha ufugaji
ng’ombe wa maziwa kilichopo katika kijiji cha Fundimbanga Tarafa ya Matemanga
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kujenga ubunifu juu
ya taratibu za ufugaji huo, ambao umeweza kuwakwamua wananchi wake kiuchumi na waweze
kuondokana na umasikini.
Pamoja na pongezi hizo,
wanachama wa kikundi hicho wameiomba pia serikali kuangalia uwezekano wa
kuwapelekea miradi mingine kama vile ufugaji wa samaki na kuku, huku wakiitaka
Halmashauri ya wilaya hiyo iwasaidie kuwajengea josho litakalosaidia kuogeshea
mifugo yao.
Hayo yalisemwa kupitia
risala yao ambayo ilisomwa na afisa mifugo wa kata ya Matemanga, Tatu Tururu na
kuongeza kuwa kijiji cha Fundimbanga kilipokea mradi wa ng’ombe wa maziwa 20
wenye thamani ya shilingi milioni 16 uliotolewa kwa ufadhili wa mpango wa DADPs,
kupitia Halmashauri ya wilaya ya Tunduru mwaka 2012.
Afisa mifugo huyo
alisema kuwa mradi huo, ulipokelewa na wanachama wa kikundi hicho cha ufugaji
ng’ombe wa maziwa kupitia kauli mbiu ya kopa ng’ombe lipa ng’ombe, ambapo kati
ya ng’ombe hao kulikuwa na majike 19 na dume mmoja.
Wanachama wa kikundi
hicho, hivi sasa wameongezeka na kufikia wanachama 42 ambapo kila mmoja wao,
sasa anamiliki ng’ombe mmoja bora wa maziwa.
Akizungumzia juu ya
changamoto ambazo wanakabiliana nazo wafugaji hao, Tururu alisema kutokana na
kukosekana kwa huduma za uhakika ikiwemo suala la kuwatibu ng’ombe wao, tatizo hilo linasababisha baadhi ya
ng’ombe kupoteza maisha na kuwafanya warudi nyuma kimaendeleo.
Pamoja na mambo mengine
akimwakilisha mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Kaimu afisa tawala wa wilaya
hiyo, Manfredy Hyera aliwapongeza wanakikundi hao kwa kujali na kutunza mradi
wao, ili uweze kuwa endelevu katika kuwaboreshea maisha yao.
Hyera alitumia nafasi
hiyo, kumtaka Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Tina Sekambo
kuangalia uwezekano wa kupanga bajeti kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani, ili
fedha zitakazopatikana zisaidie ujenzi wa josho hilo na kupeleka mtaalamu
atakayeweza kusimamia mifugo hiyo kwa karibu ili isishambuliwe na magonjwa
mbalimbali.
No comments:
Post a Comment