Gari likiwa limetumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wanafunzi
wanaosoma katika shule ya Kigonsera Catechists Secondary School (KCS) iliyopo
katika kata ya Kigonsera, akiwemo na Padri wa Parokia ya Kigonsera kanisa
katoliki jimbo la Mbinga, mkoani Ruvuma wamefariki dunia baada ya gari
walilokuwa wakisafiria, kutumbukia kwenye korongo na kuteketea kwa moto.
Wanafunzi sita na Padri
Hyasint Kawonga ndiyo waliopoteza maisha katika ajali hiyo, wakati wakitoka
shambani kuvuna mahindi yaliyokuwa yamelimwa kwa ajili ya chakula cha wanafunzi
shuleni hapo.
Padri Kawonga ndiye
Mkurugenzi wa shule hiyo, ambapo gari lenye namba za usajili T 306 AYM aina ya
Land rover ndilo walilopata nalo ajali, baada ya gari hilo kushindwa kupanda
mlima wakati wanatoka huko shambani.
Tukio hilo lilitokea
katika eneo la Minazi kata ya Kigonsera wilayani humo, Juni 4 mwaka huu majira
ya jioni ambapo baada ya kushindwa kupanda mlima katika eneo hilo, lilirudi
nyuma na kutumbukia kwenye korongo kisha kuwaka moto huku ndani ya gari wakiwa
wanafunzi na padri huyo.
Kamanda wa Polisi wa
mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kilitokana
pia gari hilo kupakia watu kupita kiasi na kwamba wanafunzi 24 walikuwa ndani
ya gari hilo, huku wengine wakiwa wananing’inia nje ya bodi la gari wakati
linatembea, wamenusurika kupoteza maisha.
Vilevile alisema kuwa
baadhi yao hali zao ni nzuri, walikuwa wakipatiwa matibabu kwenye kituo cha
afya Kigonsera na wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Wanafunzi saba kati ya
hao hali zao ni mbaya, ambapo wamekimbizwa Hospitali ya wilaya ya Mbinga kwa
ajili ya matibabu zaidi na kwamba maiti zimehifadhiwa katika kituo hicho cha
afya, ambacho humilikiwa na jimbo la Mbinga.
Majeruhi wanaopatiwa
matibabu katika hospitali hiyo ni Regobert Mahay (16), Edgar Maseko (15) Luiza
Mapunda (14), Alpha Kifaru (15), Nelly Nchimbi (16), Theodora Wolfa (16) na
kwamba Josephat Komba (16) amekimbizwa katika Hospitali ya misheni
Litembo iliyopo wilayani humo, kwa matibabu zaidi kutokana na kuungua moto
vibaya.
Msikhela alisema maiti
saba zilichukuliwa kutoka kwenye korongo hilo, ambalo linakadiriwa kuwa na
urefu wa mita tano, ambako gari lilitumbukia na kuteketea kwa moto.
Aliitaja maiti moja
ambayo imetambuliuwa kuwa ni Padri huyo na nyingine ambazo ni za wanafunzi
jitihada za kutambua majina yao zinaendelea kufanyika kutokana na kuungua moto
vibaya, hivyo kusababisha kushindwa kuzibaini kwa haraka.
“Gari hili lilikuwa
likiendeshwa na Padri Hyasint Kawonga wa kanisa katoliki Parokia ya Kigonsera,
ambaye pia ni Mkurugenzi wa shule hiyo ya KCS naye amepoteza maisha katika
ajali hii”, alisema Msikhela.
Hata hivyo taarifa
zilizotufikia hivi punde, kesho kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Ruvuma
ikiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Said Mwambungu itakwenda katika eneo la tukio
hilo ambako ajali hiyo imetokea.
No comments:
Post a Comment