Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Mihayo Msikhela. |
Na Sreven Augustino,
Songea.
NIRU Nyimbi (42) ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Mwombezi
kilichopo kijiji cha Chandarua mkoani Ruvuma, anashikiliwa na jeshi la Polisi
mkoani humo kwa tuhuma ya kumbaka mlemavu mwenye mtindio wa ubongo.
Kwa mujibu wa taarifa za tukio hilo, mtuhumiwa alinaswa akiwa
anafanya unyama huo kijijini humo ambako imeelezwa kwamba, alikwenda kufanya
kazi ya kibarua cha kufyatua tofari.
Mihayo Msikhela, Kamanda wa polisi wa mkoa huo aliwaambia
waandishi wa habari kuwa mtuhumiwa huyo alifumaniwa na mama mzazi wa binti huyo
aliyemtaja kwa jina la, Oresta Ndonde.
Mama huyo alifanikiwa kumkamata mtuhumiwa, baada ya kusikia
sauti ya binti yake akiwa analia kutokana na maumivu aliyokuwa akiyapata wakati
anafanyiwa unyama huo.
Baada ya mama huyo kusikia sauti hiyo, ambayo ilikuwa
ikitokea choo cha nyumba ya jirani yake, alikwenda haraka na kumkuta mtoto wake
akiwa amevuliwa nguo huku akiwa amelaliwa kifuani na mtuhumiwa huyo.
Alisema kuwa baada ya kushuhudia tukio hilo, mama huyo
alipiga kelele akiomba msaada ambapo majirani walijitokeza na kufanikiwa
kumkamata mtuhumiwa Nyimbi, kisha walimpeleka kituo cha polisi.
Kamanda Msikhela aliendelea kufafanua kuwa walipofika kituoni
hapo, Polisi walimpatia hati namba tatu (PF 3) kwa ajili ya kwenda kufanyiwa
uchunguzi wa afya yake hospitali, ili kuweza kubaini kama amepewa maambukizi ya
homa mbalimbali ikiwemo UKIMWI.
Hata hivyo alisema mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani, baada ya
kukamilika taratibu husika ili kupisha sheria iweze kuchukua mkondo wake na iwe
fundisho kwa wengine, wenye tabia kama hiyo.
No comments:
Post a Comment