Na Mwandishi wetu,
Songea.
ZAIDI ya vijana 60 mkoani Ruvuma, ambao hujishughulisha na
kazi mbalimbali ya kuwahudumia wateja katika maeneo yao ya kazi, wamepata
mafunzo ya kuwaongezea uelewa ambayo yametolewa na Mamlaka ya elimu na mafunzo
ya ufundi stadi (VETA) kanda ya nyanda za juu kusini, jambo ambalo litawasaidia
kuleta ufanisi mzuri katika majukumu ya kazi zao za kila siku.
Kaimu Mkurugenzi wa VETA nyanda za juu kusini, Suzan Magani
alisema mafunzo hayo yatawasaidia vijana hao kukabiliana na changamoto
mbalimbali mahali pa kazi, ambapo pia yanawaongezea uwezo wa namna ya
kuwakaribisha na kuwahudumia wateja wao.
Magani alisema kuwa Mamlaka hiyo imepewa jukumu la kutoa
mafunzo ili kuweza kukidhi mahitaji ya sekta rasmi na isiyo rasmi, kwa lengo la
kuwaongezea uwezo wadau waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na sio kwa kubahatisha,
jambo ambalo linaweza kuwarudisha nyuma kiuchumi.
Alisema katika kutoa mafunzo hayo kwenye sekta isiyo rasmi,
wamekuwa wakijenga ushirikiano na wadau hao kwa lengo la kutambua mahitaji kwa
kundi husika, kisha kuwapa mafunzo ikiwemo kozi ya kuwahudumia wateja wao.
Kozi hizo zinazotolewa hulipiwa na VETA yenyewe na washiriki
hulazimika kulipa kiasi kidogo cha gharama, ikiwa ni lengo la kutoa nafasi ya
kuweza kuwapata washiriki wengi na kuisaidia serikali katika kupunguza tatizo
la ajira hapa nchini.
Mbali na hayo, lengo lingine ni kutaka kuwawezesha wanaofanya
kazi kupata stadi wanazohitaji kwa kuboresha huduma wanazozitoa katika jamii,
ili kuongeza kipato chao.
Kwa upande wake mkufunzi, Gosbert Kakiziba alifafanua kuwa
mafunzo hayo ya kuwawezesha wadau wa huduma kwa wateja ndani ya Mamlaka hiyo
yamekuwa yakitolewa mara kwa mara ambapo sasa ni takribani miaka miwili
imepita, yalikwisha fanyika katika mkoa wa Njombe na wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma.
“Lengo halisi la kutoa mafunzo haya, ni kuwawezesha watu wa
kawaida kutambua fursa ya kukuza biashara na kuwafanya wakue kiuchumi na
hatimaye taifa letu liweze kusonga mbele kimaendeleo”, alisema Gosbert.
No comments:
Post a Comment