Na Steven
Augustino,
Tunduru.
MFUKO wa maendeleo ya jamii (TASAF) awamu ya tatu ambao kwa
sasa unatekeleza mradi wa uhawilishaji fedha kwa kaya maskini hapa nchini,
umeridhia ombi la kugharimia ujenzi wa zahanati, katika kijiji cha Tuwemacho
wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Hayo yamefuatia baada ya makubaliano yaliyofanyika, kati ya
viongozi wa mfuko huo na wananchi walioshiriki kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kijijini hapo, ambao ulilenga kuibua mradi huo na ujenzi wake kugharimu
zaidi ya shilingi milioni 75.
Kwa mujibu wa wananchi waliokuwepo katika mkutano huo, kwa
nyakati tofauti walipendekeza pia wajengewe mradi wa maji, nyumba za walimu,
vyumba vya madarasa, matundu ya choo na ghala la kuhifadhia mazao.
Akizungumzia juu ya makubaliano hayo Mkurugenzi mtendaji wa
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Tina Sekambo ambaye naye alishiriki katika
mkutano huo aliwataka wananchi hao wakati wa utekelezaji wa mradi huo,
washiriki kikamilifu kuchangia asilimia 10 wakati utekelezaji wake utakapoanza.
Sambamba na kuwepo kwa utaratibu huo, Sekambo aliwataka
kufanya mkutano mwingine wa hadhara kwa siku zijazo, kwa lengo sasa kujenga
makubaliano wapi mradi utajengwa na kufanya makubaliano ya pamoja, kutafuta
eneo ambalo halina mgogoro na halitahitaji kulipwa fidia.
Naye mshauri wa mfuko wa TASAF wilayani Tunduru, Christian
Amani aliwahakikishia wananchi hao kuwa utekelezaji wa mradi huo ujenzi wa
zahanati utaanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo, mara baada ya taratibu husika
kukamilika.
No comments:
Post a Comment