Na Steven Augustino,
Tunduru.
WAGONJWA 63 kutoka wilayani Tunduru mkoani Ruvuma, wameripotiwa
kufanyiwa upasuaji mkubwa na Madaktari bingwa, kutoka Hospitali mbalimbali
Jijini Dar es Salaam na KCMC iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Dokta Alex Kazula
alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake na
kuongeza kuwa katika matibabu hayo madaktari hao, pia waliwafanyia uchunguzi
wagonjwa 171 ambapo kati yao wengine walipewa ushauri na wengine kufanyiwa
matibabu.
Alieleza kuwa zaidi ya wagonjwa 200 walishindwa kuonana na
wataalamu hao kutokana na muda wao kwisha, pamoja na wodi za hospitali ya
wilaya hiyo kujaa na kukosekana na nafasi ya kuwahifadhi.
Dokta Kazula alisema wagonjwa waliopatiwa tiba ni pamoja na
wale ambao walikuwa wakisumbuliwa na tezi ya shingo (Goita), ngiri, kidole
tumbo na uvimbe katika mji wa uzazi.
Aidha magonjwa ambayo walikosa huduma ya matibabu kutokana na
kukosekana kwa vipimo husika, ni pamoja na wagonjwa wenye kansa mbalimbali na
kwamba wazo la kuwaleta madaktari hao bingwa lilitokana na idara yake, kutambua
uwepo wa mahitaji makubwa ya matibabu kutoka kwa wananchi wa Tunduru ambao
wengi wao, husumbuliwa na magonjwa sugu kwa muda mrefu.
Vilevile alisema wataalamu hao, ni mabingwa wa kufanya
upasuaji na tiba hasa kwa magonjwa ya wanawake ambapo juhudi za kuwaleta ni
mpango ambao ulifanywa na serikali kutokana na wilaya hiyo, kuwa pembezoni
karibu na nchi ya Msumbiji na watu wengi husumbuliwa na magonjwa hayo.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho
alipongeza jitihada zilizofanywa na madaktari hao kwa kutoa huduma hiyo ya
matibabu kwa gharama nafuu, kwa watu ambao uwezo wao wa kifedha upo chini.
No comments:
Post a Comment