Thursday, June 4, 2015

WANANCHI TUNDURU WAUKATAA MRADI VIONGOZI WAZOMEWA

Na Mwandishi wetu,
Tunduru.

WANANCHI wa kijiji cha Misechela wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wamekataa kuupokea mradi wa Uhifadhi Shirikishi wa Misitu (USM) ambao ulipangwa kutekelezwa kati yao na shirika la WWF, kutokana na madai waliyoyatoa kwamba wanahofia kunyimwa uhuru endapo mradi huo utakuwa umeanzishwa katika misitu yao.

Sambamba na kuukataa huko, wananchi hao walieleza kuwa endapo wataendela kuwalazimisha kuanzisha mradi huo kwa mabavu, wapo tayari kuchangishana fedha kwa ajili ya kupata nauli na kuteuana miongoni mwao kwenda kufikisha malalamiko yao kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Hayo yalisemwa na wananchi hao kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika kijiji hicho ambapo waliyasema mbele ya Mkuu wa wilaya hiyo, Chande Nalicho.

Walimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa, hawapo tayari kuupokea kwa kile walichodai kuwa uzoefu unaonesha kwamba wafadhili wa miradi ya aina hiyo wamekuwa wakienda kwa wananchi na maneno mazuri, lakini mwisho wa siku baada ya kuwapokea kwa mikono miwili, huwageuka na kuanza kuwanyanyasa wenyeji wao.


Nalicho ambaye alikuwa ameongozana na kamati yake ya ulinzi na usalama, alikwenda kijijini hapo kwa ajili ya kujionea hali halisi na msimamo wa wananchi hao, ambapo awali wataalamu waliokwenda kuwahamasisha juu ya uanzishwaji wake walitimuliwa kwa kupigwa mawe.

Msimamo huo wa wananchi juu ya kukataa mradi huo, ulianza kujitokeza katika kikao cha ndani ambacho kiliketi kijijini hapo chini ya Mwenyekiti wake, Jafari Kitanda ambapo walionesha kuupinga wazi wazi.

Kwenye mkutano wa hadhara, hali ya hewa iliendelea kubadilika jambo ambalo lilisababisha makundi ya vijana na wanawake kuanza kuzomea viongozi wao wa wilaya, kila walipokuwa wakijaribu kufafanua juu ya uanzishwaji wa mradi huo na faida zake.

“Mheshimiwa Mkuu wa wilaya, wafadhili wa miradi ya aina hii hufika kwetu wakiwa na maneno mazuri lakini wakisha karibishwa hugeuka na kuwa wanyama”, alisema Jafari Soto huku akitolea mfano kwa vitendo na madhara ya vifo vilivyotokea katika kijiji cha Mpombe wilayani Masasi, kutokana na vipigo walivyokuwa wakivipata kutoka kwa walinzi wa msitu wa kijiji hicho.

Akizungumza katika mkutano huo kwa masikitiko, Mkuu wa wilaya ya Tunduru Nalicho alieleza kuwa mradi huo ulianzishwa na serikali kwa lengo la kuwakwamua wananchi wake, waweze kuondokana na umaskini huku akishangazwa kwa nini wananchi hao hawautaki uanzishwe katika kijiji chao.

Mkuu huyo wa wilaya aliongeza kuwa, faida zitokanazo na misitu ni pamoja na wananchi kupasua mbao na kuziuza, kuchoma mkaa na kurina asali na kuanzisha miradi mingine mbalimbali ya ujasirimali.

Pamoja na mambo mengine, Jeremia Daffa ambaye ni mwakilishi na msemaji wa shirika la WWF naye alisema mpango huo wa uhifadhi misitu katika ukanda wa Ruvuma, unaoshirikisha hifadhi ya Niasa kwa upande wa nchi jirani ya Msumbiji utaleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo katika jamii zinazoishi katika ukanda huo.


Daffa alisema sambamba na mradi huo kuanza kutekelezwa hapa Tanzania, pia shirika hilo linatekeleza mradi huo katika nchi za Madagasca, Kenya na Msumbiji kwa lengo la kuwainua wananchi waweze kufaidi matunda ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao, huku malengo makubwa yakilenga uhifadhi wa mazingira unaojumuisha misitu, mabwawa, milima, vilima pamoja na uhifadhi wa viumbe hai ikiwemo kutunza uoto wa asili na ustawi wa jamii.

No comments: