Wednesday, June 10, 2015

HOKORORO AWATAKA VIONGOZI TUNDURU KUSAIDIA WANANCHI

Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo.
Na Steven Augustino,
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Agnes Hokororo amewataka wakuu wa idara waliopo katika wilaya hiyo kujipanga na kuanza kufanya kazi kwa weledi, ili waweze kuwasaidia wananchi wasonge mbele kimaendeleo.

Alisema kiongozi yoyote aliyepewa dhamana ya kuwaongoza wananchi wake, endapo kama anakuwa ni mtu wa kufanya kazi kwa mazoea bila kushirikisha jamii, ni hatari kwa ustawi wa maendeleo katika eneo husika.

Hokororo alisema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi hao, katika makabidhiano kati yake na aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho ambaye anahamia wilaya ya Namtumbo, ambapo pamoja na mambo mengine alisisitiza kujenga ushirikiano hasa pale atakapohitaji ushauri na maelekezo wakati akitekeleza majukumu yake.


Hokororo hivi sasa ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru, ameapa kutoa ushirikiano kwa wananchi wote wa wilaya hiyo bila kubagua.

Kwa upande wa viongozi wa dini, Mchungaji Zacharia Machinga na Shekh Mohamed Mwapetta walimpongeza mkuu huyo wa wilaya kwa kujenga msimamo huo ambao utaifanya wilaya isiweze kugawaika kwa itikadi za rangi, dini au ukabila ambapo baadaye yanahatarisha amani na utulivu.

Akihitimisha makabidhiano hayo, Mkuu wa wilaya Nalicho ambaye anahamia Namtumbo alisema uongozi ni kubadilishana hivyo anauhakika kuwa Hokororo ataisaidia Tunduru na kuifanya iendelee kusonga mbele pale alipoishia yeye.


Nalicho aliongeza kuwa, Tunduru ambayo ilizaliwa mwaka 1905 sawa na makao makuu ya nchi ya Kenya, Nairobi inahitaji kupewa msukumo wa maendeleo hasa katika sekta ya elimu, afya, maji na barabara.

No comments: