Thursday, June 4, 2015

WAFUASI WA CHADEMA MBINGA WAFIKISHWA POLISI KWA KULETA VURUGU

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

JUMUIYA ya Umoja wa Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, imewataka wanachama wa umoja huo kutojihusisha na vitendo vya vurugu hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu, badala yake watumie muda mwingi kuelezea utekelezaji wa ilani wa chama hicho, ulivyofanikiwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Hayo yalisemwa na Mhamasishaji na chipukizi wa UVCCM wa wilaya hiyo, Emmanuel Mapunda kufuatia vurugu zilizofanywa na wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwenye mkutano wa hadhara, eneo la Soko kuu Mbinga mjini Mei 31 mwaka huu.

Mapunda alisema kuwa vurugu za wafuasi hao, ambazo walizifanya wakati mkutano huo ukiendelea zilisababisha madhara ya kuumizwa kwa baadhi ya wanachama wa CCM.


Alisema vijana wa Chama Cha Mapinduzi, wanapaswa kutumia muda mwingi kuelezea namna ambavyo serikali ilivyotekeleza majukumu yake kwa wananchi walioiweka madarakani na kwa kufanya hivyo, itasaidia kwa wale wanaobeza kila jambo waweze kufahamu nini kimefanyika.

Akielezea jinsi ambavyo vurugu zilivyotokea, Mapunda alisema baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo ambao ulilenga kuelezea mafanikio ya CCM ya utekelezaji katika kipindi cha miaka kumi, ndipo ghafla walitokea vijana wa CHADEMA wakiwa wamevalia sare za chama chao na kuanza kutoa maneno ya kashfa katika mkutano huo, ambapo licha ya kikundi cha greenguard cha UVCCM kuwaomba waondoke katika mkutano huo waliendelea kubaki huku wakiendelea kutoa maneno hayo ya kashfa.

“Kufuatia vurugu hizi mkutano ulisimama kwa muda wa dakika 45 kutokana na mawe yaliyokuwa yakirushwa na wafuasi wa CHADEMA na kusababisha Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi kata ya Mbinga mjini, Sostenes Nchimbi kujeruhiwa kichwani baada ya kupigwa jiwe”, alisema Mapunda.

Baada ya vurugu hizo kuendelea kupamba moto katika eneo hilo la uwanja wa soko kuu, Mapunda alipiga simu Kituo kikuu cha polisi Mbinga mjini ambapo baadaye waliwasili askari Polisi kuja kutuliza ghasia na kufanikiwa kuwakamata wafuasi watatu wa CHADEMA, ambao walikuwa wakirusha mawe katika mkutano huo ambao haukufanikiwa kufanyika huku wengine wakitokomea kusikojulikana.

Hata hivyo mhamasishaji huyo alieleza kuwa katika vurugu hizo viti kumi vya plastiki ambavyo vilikuwa jukwaani vilivunjwa na wafuasi hao, na chanzo cha vurugu hizo kilitokana na mmoja kati ya mwanachama wa CHADEMA, Robert Kayunga ambaye ni Katibu wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) wilaya ya ya Mbinga kukihama chama hicho na kujiunga CCM.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watuhumiwa waliokamatwa wakati wa vurugu hizo kuwa ni Moris Ndomba (30), Ezekiel Mturo (30) na Astery Mapunda (23) ambao ni wafuasi wa CHADEMA wote wakiwa ni wakazi wa Mbinga mjini.

Aliwataka wanachama wa vyama vya siasa, kutoingilia mikutano isiyowahusu na kufanya fujo badala yake wahakikishe wanafuata taratibu zilizopo ili kuepuka usumbufu na kwamba viongozi wa vyama hivyo, watoe maelekezo kwa wanachama wao ili wasijiingize katika vitendo viovu hasa wakati huu ambao unatarajiwa kufanyika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.

 

No comments: