Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
MICHAEL Ndomba ambaye amebobea katika ufundi wa mitambo ya
kukoboa kahawa mbichi na kavu, ametangaza nia ya kugombea udiwani wa kata ya
Mbambi iliyopo Mbinga mjini mkoani Ruvuma, kupitia tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) huku akiahidi kuwaletea neema wananchi wa kata hiyo.
Ndomba ambaye alikuwa ni mfanyakazi wa kiwanda cha serikali
cha kukoboa kahawa wilayani Mbinga (MCCCO) tokea mwaka 1988 na baadaye
amestaafu mwaka huu, hivi sasa anafanya kazi ya mizani na ufundi wa kuunda
mitambo ya kati ya kukoboa kahawa mbichi.
“Uwezo wa kuongoza na kushughulikia matatizo ya wananchi wa
kata hii ninao, kinachotakiwa hapa ni kutumia rasilimali tulizonazo ili tuweze
kujipatia maendeleo hasa katika viwanda, kilimo na ufugaji wananchi wakizalisha
kwa wingi katika eneo hili wataweza kuondokana na umasikini”, alisema Ndomba.
Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
mjini hapa ambapo alieleza kuwa kata ya Mbambi inakabiliwa na changamoto
mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa maji na barabara za uhakika hivyo endapo
wananchi watampatia ridhaa ya kuwaongoza, atahitaji ushirikiano wa kutosha na
usimamizi mzuri wa pamoja katika kusimamia maendeleo ya wananchi ili kuleta
ufanisi wenye tija katika jamii.
Vilevile alifafanua kuwa kuhusiana na tatizo la maji na
barabara, atashirikiana na serikali kuhakikisha kwamba visima vya maji
vinachimbwa katika kata hiyo ili akina mama, waweze kuondokana na adha ya
kutafuta maji umbali mrefu na kwa upande wa barabara atahakikisha zinajengwa
kwa viwango vinavyokubalika ili ziweze kupitika wakati wote masika na kiangazi.
Kadhalika alibainisha kuwa kutokana na taaluma yake ya ufundi
aliyonayo atawaunganisha pia vijana na akina mama kwa kuwapa mbinu za kuunda
vikundi vya ujasiriamali, baadaye waweze kukopesheka na taasisi za kifedha
hatimaye waweze kusonga mbele na kuepukana na tabia ya kuwa tegemezi.
Alisisitiza kusimamia na kuboresha sekta ya elimu kwa shule
za msingi na sekondari, kwa kuwataka wazazi kupeleka watoto wao shule na
kuwapatia mahitaji muhimu ili mtoto aweze kusoma vizuri.
Hata hivyo alisema katika safari hiyo anaimani peke yake
hawezi kufika, lakini wana CCM wanachotakiwa wamuunge mkono ili aweze kuingia
madarakani na kutekeleza mambo mbalimbali ya kimaendeleo, katika kata ya Mbambi.
No comments:
Post a Comment