Vikundi mbalimbali vya ngoma za asili (kioda na mganda) navyo havikuwa mbali siku hiyo ya uzinduzi rasmi wa SACCOS hiyo. |
Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
WANACHAMA wa Chama cha ushirika cha akiba na mikopo, Litembo SACCOS wilayani
Mbinga mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kuweka akiba kwa wingi jambo ambalo
litawafanya waweze kukidhi mahitaji husika ndani ya chama hicho na kuepukana na tabia
ya kuingia mikataba ya mikopo na taasisi za kifedha, ambazo hazijapewa dhamana
ya kutoa mikopo.
Aidha wameshauriwa kwamba, endapo watahitaji kupewa mikopo hiyo ni
vyema wakaingia mkataba na benki ili waweze kupewa fedha ambazo hatimaye wataweza
kutoa mikopo kwa wanachama wake, na kuwafanya kusonga mbele kimaendeleo.
Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa benki ya CRDB tawi la Mbinga,
Efrosina Mwanja alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe ya uzinduzi wa SACCOS hiyo
iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Litembo, katika kata ya Litembo wilayani
humo.
“Ndugu zangu haki ya chombo hiki ni kuingia mikataba katika
mabenki na kuweza kupata huduma za kifedha ambazo mtakopeshana, lakini natoa
rai kwenu viongozi kuweni waaminifu ndani ya chama baadaye chama kiweze kusonga
mbele”, alisisitiza Mwanja.
Meneja huyo aliutaka uongozi wa bodi ya Litembo SACCOS kuacha
tabia ya kujilimbikizia mali kwa kujikopesha fedha wenyewe, badala yake wawe
makini na wasimame imara ili chombo hicho kiweze kuleta manufaa kwa wanachama
wote na jamii kwa ujumla.
Naye Meneja biashara wa CRDB wilayani hapa, Hando Matley
alifafanua kuwa benki hiyo ipo tayari kutoa elimu ya ujasiriamali na mikopo kwa
wanachama wa ushirika huo kwa masharti nafuu, huku akiwasisitiza kuongeza
juhudi katika kuweka akiba.
Awali akisoma taarifa ya maendeleo ya ushirika huo Makamu
Mwenyekiti, Stella Ndomba alisema kuwa wanachama wa SACCOS hiyo ni watumishi wa
Hospitali ya Litembo, ambapo mpaka sasa ina jumla ya wanachama 145 na wengine
wanaendelea kujitokeza ili waweze kujiunga ndani ya chama hicho.
Ndomba alieleza kuwa mnamo Oktoba 7 mwaka 2014 mchakato wa
kuunda chama ulianza, ikiwa ni lengo la watumishi wa Hospitali hiyo waweze
kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umaskini.
Hata hivyo alibainisha kuwa chama hicho, kimefungua akaunti
yake katika benki ya CRDB tawi la Mbinga na kukusanya fedha kutoka kwa
wanachama kwa kiingilio, hisa na amana na kufanya chama mpaka sasa kuwa na
akiba ya shilingi milioni 19,650,000.
No comments:
Post a Comment