Na Mwandishi
wetu,
Tunduru.
CHAMA cha Wananchi CUF jimbo la Tunduru Kaskazini mkoani
Ruvuma, kimemteua Manjolo Dastan Kambili kupeperusha bendera ya chama hicho
katika kuwania nafasi ya ubunge, kwenye jimbo hilo.
Maamuzi hayo yalifanywa na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama
hicho, katika uteuzi uliofanyika ukumbi wa Klasta ya walimu, tarafa ya Mlingoti
mjini hapa.
Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo kutoka
makao makuu ya CUF taifa, Abudrahaman Lugone alisema Kambili ameshinda baada ya
kupata kura 147 kati ya kura 396 zilizopigwa na kuwabwaga, washindani wake.
Alisema katika kinyang’anyiro hicho jumla ya wagombea watano,
walijitokeza kuwania nafasi hiyo ambapo nafasi ya pili ilichukuliwa na Kindamba
Mamlia ambaye alipata kura 102, Mohamed Abdallah kura 73, Issa Mtuwa kura 68 na
Issa Kapukusu aliyeshika nafasi ya mwisho kwa kupata kura 2.
Mkutano huo pia ulipitisha jina la Zuhura Kanduru kuwa
mgombea mwenza katika nafasi hiyo, na endapo Manjolo ataibuka kidedea katika
matokeo ya uchaguzi mkuu ujao basi Chipola, atakuwa Mbunge wa viti maalum
katika jimbo hilo.
Alipozungumza na waandishi wa habari, Manjolo aliwaomba
wananchi wa jimbo la Tunduru Kaskazini kumpatia ridhaa ya kuwaongoza ili aweze
kusimamia maendeleo ya wananchi katika nyanja ya elimu, afya, barabara na maji.
Mgombea huyo, pia alitumia nafasi hiyo kuwataka wapinzani
wake walioshindwa katika uteuzi huo kuvunja makundi na kumuunga mkono ili
kukiwezesha chama chao kuibuka na ushindi, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu.
Awali akizungumza katika mkutano huo Mwenyekiti wa chama
hicho cha wananchi CUF wilaya ya Tunduru, Abdalah Mtalika aliwataka wajumbe kuacha
maneno yenye ushabiki kwani kiongozi waliyemchagua wanapaswa kujenga
ushirikiano naye, ili kuweza kufikia malengo husika.
No comments:
Post a Comment