Dokta Emmanuel Nchimbi, Mbunge wa CCM jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma. |
Na Julius
Konala,
Songea.
BAADHI ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Wananchi
wa jimbo la Songea mjini mkoani Ruvuma, wamejikuta wakiangua kilio baada ya
Mbunge wa jimbo hilo, Dokta Emmanuel Nchimbi kuwatamkia rasmi kuwa hatagombea
tena nafasi ya kiti cha ubunge katika jimbo hilo.
Tukio hilo lilitokea wakati Mbunge huyo, alipokuwa
akizungumza na viongozi na wanachama mbalimbali wa CCM kuanzia ngazi ya mashina
hadi kata, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Majimaji mjini hapa.
Dokta Nchimbi aliwaambia wanachama hao kuwa ameamua kuachia
jimbo hilo, baada ya kulitumikia kwa kipindi cha miaka kumi jambo ambalo
wanachama hao wa chama tawala, walilipokea kwa mshituko mkubwa.
Baada ya tamko hilo kutolewa na Mbunge huyo wa Songea mjini,
simanzi na majonzi vilitawala katika eneo hilo la uwanja wa Majimaji, huku wengine
wakibubujika machozi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kutoamini na maamuzi
hayo magumu, ambayo yaliyotolewa na Mbunge wao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanachama hao wa Chama Cha Mapinduzi
walisema kuwa kuachia ngazi kwa Dokta Nchimbi, kutogombea kupitia jimbo hilo
kunatoa fursa kubwa kwa vyama vya upinzani kuchukua jimbo hilo, jambo ambalo
waliongeza kuwa hawatakubaliana nalo.
Wanachama hao wamemwomba Dokta Nchimbi kutengua msimamo wake,
na kumtaka arejee tena kugombea kwenye jimbo la Songea mjini ambapo Mbunge huyo
baada ya kupokea ombi hilo, aliwaeleza wanachama hao kuwa wamwachie nafasi ya
kufikiri kwanza na ifikapo Juni 28 mwaka huu, atawapatia majibu.
Awali Dokta Nchimbi katika kulitumikia jimbo lake kwa kipindi
cha miaka kumi, alielezea mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi hicho
cha uongozi wake ni pamoja na ujenzi wa barabara, zahanati, miundombinu ya maji
na shule za sekondari.
No comments:
Post a Comment