Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
UKOSEFU huduma ya uhakika ya upatikanaji wa maji safi na
salama, katika kijiji cha Mbesa wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, kuna hatarisha wakazi wa kijiji hicho kuugua homa ya matumbo, kipindupindu na kuhara kutokana na
kunywa maji machafu.
Zaidi ya wakazi 7,000 wanaoishi huko, wapo hatarini kukumbwa
na madhara hayo ambapo licha ya serikali kuweka katika mpango wa ujenzi wa
mradi wa maji ambao utagharimu shilingi milioni 700, utekelezaji wake mpaka
sasa unaonekana ukisuasua na kuwafanya wananchi wajenge hofu juu ya usalama wa
maisha yao.
Wananchi wa kijiji cha Mbesa, walipozungumza na mwandishi
wetu kwa nyakati tofauti walisema kuwa kutokana na kuwepo kwa tatizo hilo
wamekuwa wakinywa maji machafu yaliyopo kwenye vyanzo ambavyo hata wanyama
wakali kama vile simba, tembo, chuwi na nyoka wakubwa wamekuwa wakinywa maji
hayo jambo ambalo linawafanya waishi kwa hofu kubwa.
Awanda Yusuph na Zuhura Said walisema kuwa katika kipindi cha
mwaka 2013 walianza kupata matumaini baada ya serikali kupitia mradi mkubwa,
ambao unatekelezwa kwa ufadhili wa benki ya dunia na kumpatia kazi hiyo
mkandarasi wa kampuni ya Nyakile Investment Company Limited, lakini utekelezaji
wake mpaka sasa haujazaa matunda.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Ally Mchonjele amethibitisha
kwamba kijiji chake kina jumla ya wakazi 7,846 huku akikiri kuwa ni kipindi
kirefu sasa kimepita wamekuwa wakitumia maji, kutoka kwenye visima vya kienyeji
ambayo sio salama kwa afya ya binadamu.
Diwani wa kata ya Mbesa, Shaibu Kamtiko pamoja na kuonesha
mashaka juu ya ukamilishaji ujenzi wa mradi huo alisema wananchi walikuwa wakitegemea
kunywa maji kutoka kwenye visima 21 ambavyo vilichimbwa miaka ya 1980 na hivi
sasa visima vitatu tu, ndivyo vinavyofanya kazi hali ambayo inasababisha kutopatikana
kwa huduma hiyo muhimu.
Mhandisi kutoka idara ya maji wilayani Tunduru, Emmanuel
Mfinanga pamoja na kukiri kuyumba kwa maendeleo ya mradi huo alisema tayari
idara hiyo inafanya utaratibu wa kuvunja mkataba na mkandarasi huyo, kutokana
na ubabaishaji uliojitokeza katika utekelezaji wake.
Mfinanga alifafanua kuwa miongoni mwa maelekezo aliyopatiwa
mkandarasi huyo ni pamoja na kuhakikisha kwamba, anapeleka wataalamu wa kutosha
ambao wataweza kuendelea na ujenzi huo, kitendo ambacho utekelezaji wake umekuwa
hafifu.
Akizungumzia juu ya hali hiyo Mkurugenzi mtendaji Halmashauri
ya wilaya ya Tunduru, Tina Sekambo pamoja na kukiri juu ya matatizo hayo katika
mradi huo alisema halmashauri ipo katika harakati za kutafuta ufumbuzi wa
kudumu ili kumaliza kero hiyo, ambayo inawakabili wananchi wa kijiji hicho.
Sekambo alieleza kuwa mradi huo ulipangwa kugharimu jumla ya
shilingi milioni 716,539,050 na kukamilika Februari mwaka huu, na kwamba kati
ya fedha hizo tayari mkandarasi amekwisha lipwa milioni 473 kwa ajili ya ujenzi
wa tanki na banio.
No comments:
Post a Comment