January Makamba akiwa katika taswira tofauti za mapokezi na mkewe Ramona Makamba, leo mjini Songea mkoani Ruvuma. |
Na Kassian
Nyandindi,
Songea.
JANUARY Makamba, ambaye ni Mbunge wa jimbo la Bumbuli amewataka
makada wote wlioomba ridhaa ya kuteuliwa kugombea nafasi ya Urais hapa nchini, kupitia
tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) endapo kama hawana dhamira ya dhati waache
kugombea nafasi hiyo, badala yake wakiache chama kikiwa salama baada ya
kukamilika kwa mchakato huo.
Makamba alisema hayo leo mjini Songea mkoani Ruvuma, mara
baada ya kupokea orodha ya wanachama wa chama hicho ambao walijitokeza
kumdhamini ambapo jumla ya wanachama 3500 walijitokeza kumdhamini, katika
nafasi hiyo.
Alieleza kuwa kuna watu wameomba kugombea nafasi hiyo nyeti,
huku akidai kuwa baadhi yao hawana sifa na endapo hawatateuliwa, kuna hatari ya
kukisambaratisha chama hicho.
Mbunge huyo alifafanua kuwa CCM kinahitaji kupata mgombea
ambaye atahakikisha chama hicho kinabaki salama na kuwaongoza Watanzania, bila
kujali itikadi ya dini, rangi au kabila huku akijisifia kuwa yeye ndiye mwenye
uwezo wa kushika nafasi hiyo.
“Mimi siamini kwamba siasa za kupakana matope ndio zinaweza
kutujenga, sisi sote ni wanachama wa chama kimoja mwisho wa siku, tutapata
mgombea mmoja na tutahitajika kumpigia kura”, alisema Makamba.
Alisema kuwa endapo wagombea wataendelea kupakana matope
katika mchakato huu wa kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo ya urais, anaamini
wakati ukifika kumpata mteule kutakuwa na wakati mgumu kwa kile alichodai kuwa
itakuwa sio rahisi kumfanyia kampeni, mtu ambaye tayari amepakwa matope kwa
wananchi.
Kadhalika alieleza kuwa kuna kila sababu wananchi, kuwapima
wagombea ambao wanaonekana wakiomba nafasi hiyo kwa mbwembwe, kwani hata wakiipata
itakuwa ni tatizo katika kuliongoza taifa hili.
Makamba alisema kuwa CCM ni chama makini na kamwe hakitaweza
kumteua mgombea kwa uwoga, kama inavyodaiwa na baadhi ya wagombea wengine kwamba
wasipochaguliwa chama kitaingia katika hali ambaya, jambo ambalo sio sahihi.
“Nina imani kubwa kwamba chama changu kitamteua mgombea
ambaye ni mwadilifu, na ni rahisi kumnadi wakati kampeni zitakapoanza”,
alisema.
Akizungumzia juu ya mkoa wa Ruvuma, alisema mkoa huo hivi
sasa unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tatizo la upatikanaji umeme wa
uhakika na upande wa huduma za matibabu katika Hospitali ya mkoa, Songea.
Alibainisha kuwa kutokana na matatizo hayo yeye binafsi
anayatambua, endapo wananchi na chama kwa ujumla kitampatia ridhaa ya
kuchaguliwa kuwa Rais atahakikisha mkoa, unaingizwa kwenye gridi ya taifa kama
ilivyo kwa mikoa mingine.
Hata aliongeza kuwa atakapoingia Ikulu, atakuwa na uwezo wa
kuamua mambo makubwa yanayolihusu taifa hili tofauti na nafasi aliyonayo sasa
ya ubunge, ambayo inampaka wake katika kushughulikia matatizo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment