Na Muhidin
Amri,
Songea.
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, imekuwa
ikitenga kiasi cha shilingi milioni 10 kila mwaka, ikiwa ni lengo la
kuhakikisha kwamba wazee wanaoishi katika Manispaa hiyo wanapatiwa matibabu
ipasavyo, wakiwemo na wategemezi wao.
Fedha hizo zinazotengwa hugharimia matibabu ya wazee 600 na
wategemezi wao 2700, ambao hunufaika na mpango wa matibabu bima ya afya katika
zahanati, vituo vya afya na hospitali mbalimbali zilizopo katika Manispaa hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa mfuko wa afya ya jamii
mkoani Ruvuma (CHF) wa Manispaa ya Songea, Victor Nyenza alipokuwa akizungumza
kwenye mdahalo wa wazi uliohusu usalama wa wazee hapa nchini, ambao ulifanyika
mjini hapa.
Mdahalo huo ulikuwa umeandaliwa na shirika lisilokuwa la
kiserikali la PAD Nyanda za juu kusini, ambapo Nyenza alifafanua kuwa vituo vya
kutolea huduma ya afya 16 vilivyopo katika Manispaa hiyo ndivyo ambavyo vimetengwa
kwa ajili ya kutolea huduma ya matibabu kwa wazee hao.
Alisema kuwa wametengewa vyumba maalum kwa ajili ya kupatiwa
huduma husika na wagaganga wakuwahudumia, pale wanapohitaji kupatiwa tiba.
Manispaa ya Songea kwa kushirikiana na wadau wengine wa
maendeleo, imeanzisha mpango wa kugharimia matibabu hayo kwa wategemezi ambao
huwatunza wazee hao, hasa kwa wale waliokuwa chini ya umri wa maika 18 na
yatima.
Nyenza alieleza kuwa hadi kufikia mwezi Aprili mwaka huu,
tayari jumla ya kaya 1,419 za wazee wenye wategemezi 6,795 zinahudumiwa na
wamepatiwa vitambulisho vya CHF.
Alibainisha kuwa kaya 819 hupata matibabu katika vituo vya
serikali, na wazee wengine waliobakia hupatiwa huduma hiyo kwenye zahanati za
watu binafsi na mashirika ya dini.
Katika kuimarisha huduma hiyo, Manispaa ya Songea imekuwa
ikiajiri watumishi wa kutosha wa idara ya afya ili kuweza kukabiliana na
upungufu uliopo na tayari jumla ya watumishi wapya 42 wameajiriwa, kati ya hao
34 wameripoti katika vituo vyao vya kazi.
No comments:
Post a Comment