Wavuvi wakiwa katika ziwa Nyasa, wakitumia vifaa duni (mitumbwi) kuvulia samaki ambapo huhatarisha usalama wa maisha yao. |
Na Kassian Nyandindi,
Nyasa.
VIKUNDI vinavyojishughulisha na uvuvi wa samaki Mbamba bay
wilayani Nyasa mkoa wa Ruvuma, vimeutaka uongozi wa Halmashauri ya wilaya hiyo
kuchukua hatua za haraka kufanya manunuzi ya boti la kisasa la kuvulia samaki,
ambalo Ofisi ya Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda
alikwisha toa fedha kwa ajili ya kufanya manunuzi hayo.
Aidha wanakikundi hao ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini
na hujishughulisha na shughuli za uvuvi katika ziwa Nyasa, walisema kuwa
wanaushangaa uongozi wa wilaya hiyo tokea wapewe fedha shilingi milioni 14 na
ofisi ya Waziri huyo, takribani miezi miwili imepita, hakuna majibu kamilifu
waliyoyapata juu ya manunuzi ya boti hilo.
Walisema Waziri Pinda alitoa ahadi ya kununua chombo hicho cha
kisasa kwa ajili ya kuwawezesha kuvua samaki kwa urahisi, alipokuwa hivi
karibuni kwenye ziara yake ya kikazi wilayani humo baada ya kupokea kilio cha
wavuvi hao kwamba wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuzama na mitumbwi majini,
kutokana na kukosa kifaa cha kisasa cha kuvulia samaki.
“Ni muda mrefu sasa umepita hatujui kinachoendelea juu ya jambo
hili, taarifa kamili tunayo kwamba tayari Waziri mkuu alikwisha leta fedha hizi
alizoahidi kwa uongozi wetu wa halmashauri ili boti liweze kununuliwa, lakini
kila tunapofanya ufuatiliaji kwa viongozi wetu wa wilaya hakuna majibu kamilifu
tunayopewa”, walisema.
Vilevile utafiti uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa
nyakati tofauti, umebaini pia hata baadhi ya Madiwani wa halmashauri ya wilaya
ya Nyasa nao wamekuwa wakilalamikia juu ya suala hilo, na kuutaka uongozi
husika ambao hushughulikia manunuzi hayo kutekeleza suala hilo kwa haraka, ili
kuweza kuondoa malalamiko yasiyokuwa na msingi.
Madiwani hao walieleza kuwa fedha hizo za kununua boti, ofisi ya
Waziri mkuu iliziwasilisha katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma kwa ajili ya
kuzipeleka kwa Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nyasa, hatimaye taratibu
za manunuzi ziweze kuendelea.
Gazeti hili lilifanikiwa kuzungumza na Mkuu wa mkoa huo, Said
Mwambungu ambapo alikiri kupokea fedha hizo na kuongeza kuwa zimekwisha pelekwa
kwa uongozi wa wilaya hiyo, ili waweze kufanya manunuzi ya kifaa hicho cha
kuvulia samaki.
“Ni kweli tumepokea fedha hizi na tayari tumekabidhi kwa uongozi
wa Nyasa, naomba ufanye mawasiliano kwanza na Mkurugenzi wa Nyasa, atakupatia
maelezo ya kina”, alisema Mwambungu.
Hata hivyo Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo, Shaibu Nnunduma
alithibitisha kupokea shilingi milioni 14 kwa ajili ya kununua boti hilo, huku
akieleza kuwa wapo katika mchakato wa manunuzi hivyo wakati wowote kuanzia sasa
taratibu husika zitakuwa zimekamilika na wanavikundi hao kukabidhiwa chombo
hicho cha uvuvi.
No comments:
Post a Comment