Na
Kassian Nyandindi,
Songea.
WAANDISHI wa habari nchini, wametakiwa kuacha tabia ya kununuliwa
na wanasiasa kwa lengo la kuandika habari zao ambazo zimekuwa zikiegemea upande
mmoja na kusahau matatizo ya wananchi, jambo ambalo limekuwa likisababisha jamii
kukosa imani nao.
Aidha imeelezwa kuwa jamii inatambua wajibu na mchango wa
wanahabari, hivyo ni chombo muhimu
kinachopaswa kupongezwa wakati wote kutokana na kuibua mambo kadha wa kadha
ambayo yakikaliwa kimya, nchi yetu inaelekea kubaya.
Hayo yalisemwa na Wakili wa serikali mwandamizi mkoani Ruvuma
kanda ya Songea, Renatus Mkude alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wa
mkoa huo kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa habari duniani, yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Masista mjini hapa.
Mkude ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, alisema
kuwa upashanaji habari ni jambo muhimu hivyo vyombo vya habari vimekuwa
vikijenga ustawi mkubwa wa maendeleo katika jamii na kwamba, kukua kwa
tekinolojia duniani kumesaidia pia wananchi kupata habari kwa wakati na ubora
wa hali ya juu.
“Ndugu zangu utawala wa sheria sio nchi tu kufuata sheria, bali
kuwepo kwa sheria zinazozingatia haki hivyo nawasihi hata ninyi katika
utekelezaji wa majukumu yenu ya kila siku zingatieni taratibu na sheria za kazi
zenu, kwa kuitendea haki jamii hii ambayo inawazunguka”, alisema Mkude.
Vilevile alieleza kuwa waandishi wa habari waepuke kuandika habari
za uzushi, ili kuepukana na machafuko yanayoweza kutokea baadaye ambapo
wazingatie maslahi ya nchi na watu wake, kwa kufanya kazi zao kwa weledi.
“Nawasihi endeleeni kuibua maovu ili tuweze kuleta maendeleo,
andikeni habari sahihi tuweze kujenga uwazi na wajibikaji katika jamii pia
jengeni utamaduni wa kushirikiana na serikali, kuiwezesha kutimiza malengo
yake”, alisema.
Hata hivyo aliongeza kwa kuwataka wanahabari, kutumia kalamu zao
kuelimisha jamii juu ya mambo mtambuka na namna ya kupambana nayo, kama vile
vita dhidi ya rushwa na utunzaji wa mazingira.
No comments:
Post a Comment