Na Julius Konala,
Songea.
WAHITIMU wa chuo cha
Sayansi na tekinolojia ya mawasiliano cha Mtakatifu Joseph, kilichopo katika
Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wametakiwa huko waendako kutumia vyema elimu
waliyoipata, kwa malengo ya kuwakomboa Watanzania na taifa kwa ujumla.
Aidha wameshauriwa
kutumia kipawa walichonacho, kuongeza juhudi na maarifa waliyoyapata chuoni
hapo ili waweze kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii, kwa manufaa ya kizazi
cha sasa na baadaye.
Rai hiyo ilitolewa na
Askofu Mkuu wa jimbo kuu katoliki la Songea, Damian Dallu alipokuwa akizungumza
na wanafunzi, wazazi na walimu kwenye mahafali ya sita ya chuo hicho
yaliyofanyika mjini hapa.
Wahitimu zaidi ya 100
walitunukiwa vyeti vya stashahada na shahada na kwamba alipongeza uongozi wa
chuo kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania, kwa kutoa mchango wake mkubwa kwenye
nyanja ya elimu hapa nchini huku akiwataka wananchi kutumia chuo hicho kupata
elimu bora zaidi, ambayo itasaidia taifa kupata wanasayansi wengi zaidi.
Kwa upande wake Mkuu wa
chuo hicho Tanzania, Padri Arulraj ameipongeza serikali ya awamu ya nne chini
ya uongozi wa Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, Dokta Jakaya Kikwete na
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) pamoja na wadau mbalimbali wa elimu,
kwa kutoa michango yao ambayo imesaidia kukua kwa chuo hicho.
Vilevile Rais wa chuo
cha Mtakatifu Joseph Afrika, Dokta Ananth alisema mbegu njema iliyopandwa
katika ardhi ya Tanzania mnamo mwaka 2003 imeweza kuzaa matunda mazuri kutokana
na kufanikiwa kupata chuo kikuu, na kuongezeka kwa vyuo vitano vyenye jumla ya
wanafunzi 8,000 hapa nchini.
Dokta Ananth alisema
kuwa katika kipindi hiki cha mwaka 2015 wanatarajia kuanzisha vyuo vingine
viwili, katika maeneo ya Sumbawanga na Boko Jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti na mwandishi wa habari hizi, wahitimu waliokuwepo kwenye mahafali hayo
walielezea furaha yao wakisema watahakikisha elimu waliyoipata wanalisaidia
taifa hili, hasa katika kipindi hiki cha ulimwengu wa sayansi na tekinolojia
huku wakiiomba serikali kuwatumia pale zinapotokea fursa mbalimbali, hususani
katika uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura (BVR).
No comments:
Post a Comment