Na Kassian Nyandindi,
Dar
es Salaam.
IMEELEZWA kuwa watumishi wa umma kwa kushirikiana na watu binafsi
hapa nchini, baadhi yao wamekuwa hawafuati taratibu ambazo zinaongoza
manunuzi katika sekta ya umma, kitendo ambacho kimekuwa kikisababisha kuathiri ustawi
wa maendeleo ya wananchi.
Aidha imeshauriwa kuwa uadilifu na uwazi katika kusimamia mfumo wa
manunuzi ya umma ni jambo ambalo linapaswa kuzingatiwa wakati wote, ili
kuwezesha upatikanaji wa thamani halisi ya fedha na matokeo yenye tija kijamii
na kiuchumi.
Hayo yalisemwa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya fedha, Dorothy
Mwanyika ambaye alikuwa akimwakilisha Naibu Waziri wa fedha, Mwigulu Nchemba
katika semina ya siku moja iliyowakutanisha Waandishi na wadau wa habari.
Semina hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi
Tanzania (PPRA) ambayo pia inaadhimisha miaka kumi tokea ianzishwe hapa nchini,
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee Jijini Dar es Salaam.
“Katika kuandika habari za manunuzi ya umma waandishi wa habari
mnao mchango mkubwa sana, kumekuwa na malalamiko mengi juu ya ubadhirifu katika
sekta hii, nawasisitiza endeleeni na mchango wenu wa kuibua maovu yanayofanywa
katika sekta hii, ili muweze kujenga uwazi na uwajibikaji”, alisema Mwanyika.
Kadhalika alipongeza jitihada zinazofanywa na waandishi wa habari
hapa nchini, katika kuripoti habari za maendeleo ya wananchi hasa kwa upande wa
manunuzi ambako kwa kiasi kikubwa baadhi ya watumishi, katika taasisi husika au
kamati za Halmashauri za wilaya wamekuwa wakitekeleza miradi chini ya kiwango.
Naibu katibu mkuu huyo alifafanua kuwa vitendo vya rushwa,
ubadhirifu na malipo hewa yamekuwa yakifanyika katika maeneo mbalimbali na
kusababisha kuwepo kwa malalamiko mengi kutoka kwa wadau, hivyo kusababisha
hata ustawi wa maendeleo katika taifa hili kurudi nyuma kutokana na watumishi wasio
waaminifu kutekeleza majukumu yao, kwa kutozingatia taratibu za utumishi wa
umma.
Awali kwa upande wake Afisa mtendaji mkuu wa PPRA, Dokta Laurent
Shirima alieleza kuwa Mamlaka hiyo tokea ianze kufanya kazi zake hapa nchini,
tayari imekwisha yafungia kampuni 26 na kuyakataza kutofanya kazi tena ya
manunuzi ya umma kutokana na kukiuka sheria, kanuni na taratibu husika.
“Ndugu zangu manunuzi ya umma sio kichaka cha watu kujitafutia
fedha isiyo halali, tunahitaji taratibu zifuatwe kumekuwa na tatizo la kukosa
uadilifu katika manunuzi, wizi, kukosekana kwa uadilifu na vitendo vya rushwa
katika shughuli nzima ya kufanya manunuzi, mamlaka tutaendelea kupambana na
mambo maovu haya”, alisema.
Dokta shirima aliongeza kuwa uzingatiaji wa haki, ushindani,
uwazi, kutokuwepo kwa ubaguzi na upatikanaji wa thamani wa manunuzi ya umma
ndio mambo muhimu, ambayo yanapaswa kuzingatiwa wakati wote.
Hata hivyo alifafanua kwamba, PPRA itaendelea kuzingatia viwango
na ufuatiliaji wa sheria husika, kwa taasisi za ununuzi ikiwemo kuratibu,
kuanzisha na kusimamia mfumo wa manunuzi kwa kutumia tekinolojia ya TEHAMA.
No comments:
Post a Comment