Na Julius
Konala,
Songea.
MAFUNDI rangi waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya
Songea mkoani Ruvuma, wamenufaika na mafunzo juu ya utumiaji wa tekinolojia ya
upakaji rangi ikiwa ni lengo la kuwajengea uwezo, utendaji wa kazi zao za kila
siku.
Zaidi ya mafundi 100 ndio waliopewa mafunzo hayo na kampuni
ya Gold Star katika Manispaa hiyo, ambayo yalifanyika kwa muda wa siku moja
kwenye ukumbi wa chuo cha Top one inn, mjini Songea ambayo yalishirikisha
wanawake na wanaume.
Akizungumza katika mafunzo hayo Meneja mauzo wa kampuni hiyo,
Ally Khalfan alisema kuwa lengo ni kuboresha taaluma ya upakaji rangi kwa
mafundi hao, ili kuweza kuleta mabadiliko katika utendaji wa kazi zao.
Meneja huyo alieleza kuwa mafundi wengi hapa nchini, wamekuwa
wakifanya kazi ya upakaji rangi kienyeji na kwa kiwango cha chini bila
kuzingatia vigezo husika, jambo ambalo kampuni yake lilimfanya aweze kujenga
msukumo wa kuendesha mafunzo hayo ili mafundi hao waweze kujiajiri wao wenyewe
katika shughuli mbalimbali za upakaji rangi, pale zinapojitokeza na kwa viwango
vinavyokubalika.
Naye Mkurugenzi wa chuo cha Top one inn kilichopo mjini hapa,
Paschal Msigwa aliwataka washiriki wa mafunzo hayo huko waendako mara baada ya
kupatiwa ujuzi huo wa namna ya upakaji rangi, wakafanye mabadiliko sahihi katika
kazi zao ambayo yataleta faida kwao na taifa kwa ujumla.
Awali alipokuwa akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Meya wa
Manispaa ya Songea, Diwani wa kata ya Mshangano mjini hapa, Faustine Mhagama
aliishukuru kampuni ya Gold Star kwa uamuzi wake wa kuwajengea uwezo mafundi
rangi kwa kile alichoeleza kuwa, ni nafasi pekee itakayowafanya wengi wao
waweze kujiajiri wenyewe.
Mhagama alisema kuwa elimu waliyoipata huko waendako,
wakiitumia vizuri itaweza kusaidia na kuboresha upakaji rangi katika nyumba na
majengo mbalimbali kwa viwango vinavyokubalika, badala ya kufanya kazi kienyeji
kama ilivyokuwa hapo awali.
No comments:
Post a Comment