Na Mwandishi
wetu,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imeapa kutofumbia
macho kitendo chochote kitakachojitokeza juu ya uvunjifu wa amani katika zoezi
la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, ambalo hivi sasa linaendelea
wilayani humo.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilayani hapa,
Chande Nalicho ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru alitoa rai hiyo
alipokuwa akizungumza hivi karibuni, katika maadhimisho ya sherehe za
wafanyakazi zilizofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
uliopo mjini hapa.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa wilaya alisema kwamba, amechukua
hatua ya kutoa tamko hilo kufuatia taarifa za kiintelejensia ambazo zimemfikia
ofisini kwake kuwa, kuna mbinu chafu zinasukwa chini kwa chini na watu wenye
nia mbaya kwa lengo la kutaka kuleta vurugu ili zoezi hilo lisiweze kufanikiwa
kama ilivyopangwa.
“Kuna taarifa tumepata kuwa kuna kundi la vijana ambao
wanafadhiliwa na vyama vya upinzani, wanataka kutuharibia zoezi hili kwa vurugu
wanazotaka kuzianzisha ambazo hazina msingi wowote, sasa wakifanya hivyo hakika
na waambieni serikali haitalifumbia macho jambo hili watakiona chamtemakuni”,
alisema Nalicho.
Nalicho alifafanua kuwa vijana hao wanataka kuwazuia wazee
katika vituo hivyo vya kujiandikisha ili wasijiandikishe, kwa madai kwamba
wamekuwa wakiwachagua viongozi wa CCM katika chaguzi mbalimbali ambao hawawaletei
maendeleo.
Awali akizungumzia juu ya maadhimisho ya sherehe za
wafanyakazi, Mkuu huyo wa wilaya aliwataka waajiri kuachana na tabia ya
kuwatumikisha watumishi wao bila kuwapatia maslahi yao, badala yake watimize
wajibu wa kutoa haki zinazostahili ili kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya
kazi.
Naye Katibu wa Muungano wa shirikisho la vyama vya
wafanyakazi (TUCTA) wilayani Tunduru, Kassim Dini aliwataka viongozi wilayani
humo kubadilika katika utendaji wa kazi zao na kuiga mfano mzuri unaofanywa na
viongozi wa kitaifa, katika kutatua kero za wafanyakazi kwa haraka.
Dini alieleza kuwa endapo Halmashauri ya wilaya hiyo,
itaendelea kupuuza kero mbalimbali za wafanyakazi wake wilayani humo ni
kuendelea kukuza migogoro mahali pa kazi isiyokuwa ya lazima, jambo ambalo
litasababisha ufanisi wa kazi maofisini kushindwa kufikia malengo husika.
No comments:
Post a Comment