Thursday, May 7, 2015

WASHAURIWA KUJIUNGA NA HUDUMA YA MATIBABU NIHF

Na Muhidin Amri,
Songea.

VIONGOZI wa vyama vya akiba na mikopo mkoani Ruvuma, wameombwa kusaidia wanachama wao kujiunga na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NIHF) ili waweze kupata huduma bora ya matibabu pale wanapougua, badala ya kutembea na kiasi kikubwa cha fedha mifukoni kwa lengo la kwenda kupata matibabu katika hospitali mbalimbali. 

Aidha wameaswa kuwa waaminifu na waadilifu kwa wanachama wao, katika kuwaongoza na kuacha ubadhirifu wa fedha na mali zao katika chama ambapo kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanachama wanashindwa kuendelea kujiunga katika vyama hivyo na kubaki wakikata tamaa.


Rai hiyo ilitolewa na Meneja wa shirika hilo mkoani Ruvuma, Slivery Mgonza alipokuwa akizungumza na wanachama wa vyama vya akiba na mikopo wilaya ya Songea, huku akiwakumbusha umuhimu wa kujiunga na mfuko huo.

Mgonza alisema serikali nchini, imedhamiria kuwasaidia wananchi wake katika kupambana na vita dhidi ya adui maradhi na kwamba ni muhimu kwa kila mwananchi kujiunga na mfuko wa NIHF, ili aweze kunufaika nao.


Alisema mpango huo umefika kwa wakati muafaka, kutokana na sasa kumekuwa na kila aina ya magonjwa ambayo hushambulia binadamu na kusababisha wengine kupoteza maisha, kutokana na kukosa matibabu bora.

No comments: