Baadhi ya wananchi wakishuhudia basi la kampuni ya Babu J Trans, likiteketea kwa moto baada ya kuchomwa na wananchi wenye hasira kali. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
SERIKALI wilayani
Tunduru mkoa wa Ruvuma imeapa kwamba, haitawasamehe wananchi wa kijiji cha
Mhuwesi na Msagula wilayani humo ambao wamehusika kuchoma moto basi la kampuni
ya Babu J Trans, na kuliteketeza kabisa kutokana na basi hilo kugonga mtoto na
kufariki dunia papo hapo.
Chande Nalicho ambaye ni
Mkuu wa wilaya hiyo, alisema hayo alipokuwa katika eneo la tukio kwa lengo la
kujionea uharibifu huo uliofanywa na wananchi wenye hasira kali kwa
kujichukulia sheria mkononi, kinyume na taratibu za nchi zinavyotaka.
Mkuu huyo wa wilaya
alilaani vikali kitendo hicho, baada ya basi hilo kumgonga mwanafunzi
aliyefahamika kwa jina la Faidhi Ally (10) na kusababisha kifo papo hapo,
katika ajali iliyotokea Mei 26 mwaka huu majira ya mchana.
Alisema serikali haiwezi
kuendelea kuvumilia matukio kama hayo ya uvunjifu wa amani, akidai kuwa ni
tukio la tatu sasa kwa wananchi wa maeneo hayo kutekeleza kitendo cha aina
hiyo, pale inapotokea ajali kwa kugongwa mtu na kusababisha kifo.
Baadhi ya wananchi wa
vijiji hivyo, walikiri kwa nyakati tofauti kushiriki kwa namna moja au nyingine
kulichoma moto basi hilo ambalo ni aina ya TATA lenye namba za usajili, T 841
DDL huku wakiiomba serikali iwasamehe juu ya tukio hilo kwamba hawatarudia
tena.
Kamanda wa Polisi wa
mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela alisema wamejipanga kuhakikisha wanafanya
uchunguzi wa kina ili kubaini watuhumiwa wote waliohusika, wanakamatwa na
sheria iweze kuchukua mkondo wake.
“Hawa wananchi wenye
hasira kali baada ya tukio kutokea, walivamia abiria na kuwaamuru washuke
watoke nje ya basi hilo na baadaye kulichoma moto, huku dereva na watu wengine
walilazimika kukimbia”, alisema Msikhela.
Kwa mujibu wa abiria
waliokuwa wakisafiri na gari hilo, kutoka Songea mkoani Ruvuma kuelekea wilaya
ya Masasi Mtwara walisema ajali hiyo ilitokana na uzembe wa marehemu, baada ya
kuvuka barabara ghafla wakati basi hilo likipishana na lori ambalo lilikuwa
likivuta tela.
No comments:
Post a Comment