Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Njenga katika maadhimisho ya siku ya Malaria Africa. |
Na Steven Augustino,
Tunduru.
IMEELEZWA kuwa asilimia 38.3 ya vifo vilivyotokea mwaka
2014 wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, vilitokana na ugonjwa hatari wa Malaria.
Hayo na mengine mengi, yalibainishwa katika taarifa iliyosomwa na mratibu msaidizi wa ugonjwa huo wilayani humo, Ayub Joseph katika
maadhimisho ya siku ya Malaria Africa yaliyofanyika kijiji cha Njenga
wilayani humo.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa siku hiyo, jumla ya watu
487 waliripotiwa kupoteza maisha katika vituo vya kutolea huduma za afya
wilayani Tunduru.
Akizungumzia mkakati wa kupambana na ugonjwa huo, Joseph
alisema pamoja na uwepo wa juhudi hizo za kupambana na Malaria idara yake
imekuwa ikikabiliana na changamoto ya upatikanaji wa madawa na vifaa tiba, ambavyo
mgawo wake umekuwa ukitolewa bila kuzingatia uwiano na bohari ya dawa hapa
nchini (MSD).
Joseph alifafanua kuwa katika kipindi hicho, pia vituo vyake
vya afya wilayani humo, vilitoa huduma kwa wagonjwa wa nje 10,791 ambao
waligundulika kuugua Malaria.
Takwimu ziliendelea kufafanua kuwa, kati ya wagonjwa 10,503
walipokelewa na kulazwa katika vituo vya afya, zahanati na hospitali ambazo
zipo katika wilaya hiyo, kati ya hao wagonjwa 5,893 walibainika kuwa na
ugonjwa huo.
Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Nalicho aliwataka wananchi mara kwa mara kutunza
mazingira yao katika hali ya usafi ili waweze kuondokana na mazalia ya mbu,
ambao hueneza ugonjwa huo.
Sambamba na kuyatekeleza hayo, aliwasihi waachane na mila
potofu kwenda kwa waganga wa kienyeji hasa pale wanapojisikia wana homa kali,
badala yake waende hospitali au katika vituo vya afya ambavyo vimewekwa na
serikali, kwa ajili ya kuhudumia wananchi wake.
No comments:
Post a Comment