Na Steven
Augustino,
Tunduru.
DEREVA mmoja ambaye amekuwa akiendesha magari makubwa ya mizigo
na hufanya safari zake katika maeneo mbalimbali hapa nchini, amefariki dunia
katika ajali iliyotokea kona ya mbwa eneo la Nakayaya, karibu na kiwanda cha
kubangua korosho wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma.
Said Jiram (37) ndiye aliyefariki dunia ambapo ndani ya gari
alilokuwa akiliendesha lenye namba za usajili T 481 ATZ aina ya Toyota Carina
ambalo ndani yake alikuwa na wenzake wawili, ambao walinusurika kifo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, walieleza kuwa watu
hao walipatwa na mkasa huo wakati walipokuwa wakielekea karibu na kiwanda
hicho, kwa lengo la kwenda kupakia korosho kwenye lori hatimaye wasafirishe
kwenda Jijini Dar es Salaam.
Akifafanua juu ya tukio hilo rafiki wa marehemu huyo, Mohamed
Mponda ambaye ni mmoja aliyenusurika kwenye ajali hiyo alisema kuwa yeye na
marehemu walikuwa pamoja kwenye gari hilo, ambapo wakiwa njiani kuelekea huko ghafla
gari lilipinduka mara mbili na kusababisha kifo kutokana na Jiram kupatwa na
majeraha mengi mwilini huku akitokwa na damu nyingi.
Mohamed alifafanua kuwa baada ya tukio hilo aliomba msaada wa
gari kwa kampuni ya Kichina (CCECC) ambayo ipo katika barabara hiyo ya Tunduru,
ikifanya kazi ya kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami ambapo walimkimbiza
katika hospitali ya wilaya, kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Walipofika hospitalini hapo licha ya matabibu kufanya
jitihada ya kuokoa uhai wake hawakufanikiwa, ambapo alikata roho muda mfupi wakati
akiwa mikononi mwao wakiendelea kumpatia matibabu.
Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo kilisababishwa na
mwendo kasi, hali ambayo ilisababisha marehemu kushindwa kumudu gari hilo na
kumfanya kuyumba nalo kukosa mwelekeo kisha kupinduka.
Hata hivyo Mganga aliyeufanyia mwili wa marehemu Jiram, Dokta
Andreas Ndunguru alisema kifo hicho kilitokana na kutokwa na damu nyingi baada
ya kupata mpasuko wa ndani kwa ndani, katika fuvu la kichwa chake.
No comments:
Post a Comment