Na Muhidin Amri,
Namtumbo.
KATA tano zilizopo katika Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo
mkoani Ruvuma, zimefanikiwa kuandikisha watu 30,832 katika daftari la kudumu la
wapiga kura idadi ambayo imeelezwa kuwa ni moja kati ya mafanikio makubwa
wakati zoezi hilo likiendelea kutekelezwa wilayani humo.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Mkurugenzi mtendaji
wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Alli Mpenye alisema katika awamu ya kwanza zoezi
hilo lilihusishwa katika kata tano za Mgombasi ambapo watu waliojiandikisha
walikuwa 5,186, Namtumbo 9,041, Likuyu 4,952, Rwinga 7,586 na kata ya Luegu
watu waliojiandikisha walikuwa 4,064.
Mpenye alifafanua kuwa hivi sasa wanaendelea na kata
nyingine, na kwamba wamelazimika kufanya kwa wamu kutokana na ufinyu wa vifaa
ikiwemo mashine ya kuandikishia wapiga kura (BVR) ambapo baadhi yake
zilizoletwa na tume ya taifa ya uchaguzi ni mbovu na hushindwa kufanya kazi
ipasavyo na kulazimika kutumia mashine chache zilizopo ambazo hufanya kazi.
Alieleza kuwa baada ya kumaliza kazi hiyo ya uandikishaji
katika kata hizo, zoezi hilo litaendelea tena katika kata ambazo zipo pembezoni
mwa wilaya hiyo ambazo ni Ligera, Lusewa, Mgazini na kata ya Msisima.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, awali kazi hiyo ilianza kwa
kusuasua kwa kile alichoeleza kuwa mwitikio mdogo wa wananchi wenyewe na baada
ya kuwafikia taarifa za kutosha katika maeneo yao, ndipo walianza kujitokeza
kwa wingi.
Asasi za kiraia, wananchi na vyama vya siasa, Mpenye
amevipongeza kwa jitihada yao ya kupita kuhamasisha zoezi hilo ili watu
wakajiandikishe na ndio maana wengi wao hivi sasa katika vituo husika wilayani
humo, wanahamasa kubwa ya kutekeleza zoezi hilo ili utakapofika uchaguzi mkuu
ujao waweze kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemataka awaongoze, kwa
nafasi ya Rais, Mbunge na Diwani.
No comments:
Post a Comment