Na Steven
Augustino,
Tunduru.
FAMILIA ya Athuman Mbwana, wa kijiji cha Nambalapi kata ya
Masonya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma inawaomba wasamaria wema kutoa msaada
wa kuwawezesha kulea watoto wao watatu, ambao walizaliwa kwa wakati mmoja ndani ya
familia yao.
Mbwana alitoa ombi hilo, alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu baada ya wauguzi na wakunga wa Hospitali ya wilaya hiyo, kumtaarifu kuwa mkewe
kipenzi Rehema Rashid ambaye alipelekwa hospitalini hapo akiwa mjamzito,
kajifungua watoto hao kwa mpigo.
Aidha anaiomba serikali na taasisi binafsi kuwa na jicho la
huruma, ili waweze kumsaidia kutunza watoto hao kutokana na yeye binafsi kuwa
na kipato kidogo cha kumwezesha kuishi.
Alisema kupata watoto hao ni neema ya mwenyezi Mungu, na
matokeo hayo hayakuwa matarajio yake hivyo anaomba msaada wa hali na mali ili
aweze kuwatunza na kuwapatia mahitaji muhimu, ambayo yatawafanya waishi na kukua
vizuri.
Naye Mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya ya Tunduru, Dokta
Mmari Zabron alithibitisha kuzaliwa kwa watoto hao watatu huku akiongeza kuwa
Mama wa watoto hao alijifungua kwa njia ya upasuaji, watoto wakiwa na afya
njema.
Mmari alifafanua kuwa mtoto wa kike wa kwanza kuzaliwa, alikuwa
na uzito wa kilogramu 1.8 wa pili kilogramu 2.1 na mtoto wa mwisho ambaye
alikuwa wa kiume alikuwa na uzito wa kilo 2.5.
Kadhalika alifafanua kuwa, watoto hao ambao kati yao walikuwa
wa kike wawili na wa kiume mmoja baada ya kujiridhisha na maendeleo ya afya ya
mama yao, uongozi wa Hospitali hiyo wakati wowote utamruhusu arejee makwao ili
akaendelee na malezi ya familia yake.
Tunaomba kwa yule atakayeguswa na jambo hili, anaweza kutoa
msaada wake kwa mawasiliano ya kupitia simu namba; 0786 041017 au 0689 595213.
No comments:
Post a Comment