Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
WANANCHI wilaya ya Tunduru mkoani hapa, wamehimizwa kupeleka
watoto wao katika vituo vya kutolea huduma za afya ili waweze kupatiwa chanjo
za magonjwa pingamizi, katika ukuaji wa watoto hao.
Chande Nalicho alitoa rai hiyo wilayani humo, wakati wa zoezi
la uzinduzi wa wiki ya utoaji wa chanjo duniani, ambalo Tunduru lilifanyika
katika viwanja vya hospitali ya serikali ya wilaya hiyo.
Aidha Mkuu huyo wa wilaya, aliwataka akina mama ambao
walijitokeza katika zoezi hilo kuwa wajumbe wa kusambaza taarifa kwa wenzao,
ili kuweza kuhamasisha jamii iweze kujitokeza kwa wingi na kupatiwa huduma
hiyo.
Pamoja na mambo mengine, akisoma taarifa ya uzinduzi wa siku
ya chanjo duniani katibu wa afya wilayani Tunduru, Maria Mzena alisema kuwa chanjo
hizo ni muhimu hivyo jamii inapaswa kushiriki kikamilifu.
Mratibu wa chanjo wilaya ya Tunduru, Rozi Jemeni alisema
kwamba mwaka huu idara yake imejipanga na kuhakikisha kuwa inatekeleza zoezi
hilo, kwa asilimia 100 ikiwa ni tofauti na chanjo zilizofanyika mwaka jana
ambapo wilaya ilichanja watoto kwa asilimia 93 tu.
No comments:
Post a Comment