Na Steven Augustino,
Tunduru.
Ramadhan Ayubu (48) ambaye ni mchimbaji wa madini ya vito vya
thamani, katika kijiji cha Mitwana kata ya Lukumbule wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma, amefariki dunia baada ya kuangukiwa na kifusi.
Shuhuda wa tukio hilo, Mbangu Eliasi alieleza kuwa lilitokea
Mei 9 mwaka huu majira ya asubuhi wakati walipokuwa, wakiendelea na kazi ya
uchimbaji.
Eliasi alifafanua kuwa wakati tukio linatokea kila mmoja alikuwa
akichimba katika shimo lake yeye na marehemu, ambapo ghafla alisikia kishindo
kikubwa na kufuatiwa na ukimya uliotawala kwa muda mrefu kati yake na mwenzake,
hali ambayo ilimfanya atoke haraka nje katika shimo lake na kwenda kumuangalia
mhanga huyo kama yupo salama.
“Mimi na marehemu tulikuwa tunachimba katika mashimo ambayo
yalikuwa yamekaribiana, tulikuwa tunazungumza lakini ghafla niliona kimya na
kila nilipokuwa nikijaribu kuzungumza naye sikupata majibu”, alisema.
Alisema baada ya kuona ukimya huo, alitoka katika shimo lake
na kwenda kumuangalia mwenzake alipofika alishuhudia lundo la udongo likiwa
limeanguka katika shimo ambalo Ramadhan alikuwa akichimba, jambo ambalo
lilimfanya apige kelele kuomba msaada zaidi.
Baada ya tukio hilo na mara alipopiga mayowe, ndipo
walijitokeza wachimbaji wengi na kusaidia kufukua shimo hilo na kufanikiwa
kuukuta mwili wa marehemu huyo, na baadaye waliutoa nje ya shimo hilo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Ruvuma, Mihayo Msikhela
amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kueleza kuwa mwili wa marehemu,
umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya kukamilika uchunguzi.
Msikhela amewataka wachimbaji wa madini mkoani Ruvuma,
kufanya shughuli zao wakiwa wanalindana ili kuweza kuokoa maisha yao kwa haraka,
hasa pale yanapotokea matukio ya mtindo huo.
Hata hivyo, ameitaka idara ya madini kutembelea maeneo yote
ya wachimbaji wadogo wadogo mkoani humo, kwa lengo la kutoa elimu juu ya
uchimbaji salama ili wasiweze kupoteza maisha yao.
No comments:
Post a Comment