Na Julius Konala,
Namtumbo.
WAKULIMA wanaozalisha zao la mpunga wilayani Namtumbo mkoa wa
Ruvuma, wamenufaika na elimu ya matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo na
upandaji wa zao hilo katika mashamba darasa, yanayoendeshwa na taasisi isiyo ya
kiserikali ya Briten kupitia ufadhili wa shirika la kuleta mapinduzi ya kijani
barani Afrika, AGRA.
Zaidi ya wakulima 2,660 ndio walionufaika na mpango huo, ambapo
Mratibu wa kitengo cha shamba darasa na mtaalamu wa kilimo cha zao la mpunga
wilayani humo, Saamy Mwakyusa alisema hayo kwenye uzinduzi wa siku ya mkulima
kiwilaya iliyofanyika kijiji cha Namtumbo mbele ya Mkurugenzi wa wilaya hiyo,
Ally Mpenye.
Mwakyusa alisema kuwa, elimu hiyo ambayo wameipata wakulima wake
imeleta tija kwa madai kwamba jumla ya mashamba darasa 76 katika vijiji vya
wilaya hiyo, vimeonyesha kufanya vizuri na wakulima wengi wamepata mafunzo ya
kilimo hifadhi ya udongo.
Mmoja wa wakulima bora kutoka katika kijiji cha Namtumbo, Gerold
Haulle aliipongeza taaisisi ya Briten kwa kuwapa elimu hiyo pia yakiwemo na
mafunzo ya mawakala wa usambazaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima, ambapo
kufanya hivyo kumeweza kusaidia kuongeza uzalishaji na kipato kwa ngazi ya
familia.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya
Namtumbo, Ally Mpenye alipongeza jitihada hizo ikiwemo na benki ya CRDB kwa
kuwawezesha wakulima hao, kuwapatia tekinolojia ya kilimo bora na cha kisasa.
Aidha Mpenye aliwaasa wakulima kusindika mazao yao katika ubora na
usalama, kwa lengo la kukabiliana na ukosefu wa masoko pamoja na walanguzi
ambao wamekuwa wakiwanyonya kwa kununua mazao kwa bei ya chini na kumfanya
mkulima, kushindwa kunufaika huku akiendelea kubaki katika hali ya umaskini.
Pamoja na mambo mengine Mratibu wa Briten nyanda za juu Kusini,
Ainea Mgulambwa alifafanua kuwa lengo kuu la mradi huo ni kusambaza tekinolojia
ya kilimo bora kwa wakulima, ili waweze kuongeza uzalishaji na kipato katika
maisha yao na kwamba taasisi hiyo imekwisha fanikiwa kufikisha tekinolojia
husika katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo wilaya ya Ludewa, Kilolo,
Songea na Namtumbo.
No comments:
Post a Comment