Na Steven
Augustino,
Tunduru.
MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho
amewajia juu na kuwataka wananchi wa wilaya hiyo kujenga tabia ya kufanya usafi
katika nyumba zao wanazoishi, ikiwa ni pamoja na kufua vyandarua vyao
wanavyojifunika wakati wanapolala ili kuweza kuepukana na wadudu aina ya
kunguni, ambao muda mwingi wamekuwa wakilalamika huwauma nyakati za usiku.
Aidha akatumia nafasi hiyo, kuwataka wananchi hao kupeleka
watoto wao shule ili wakapate elimu ambayo itawawezesha kujitambua na
kupambanua mambo, katika maisha yao ya kila siku na sio muda mwingi kuutumia
kulalamika.
Hali hiyo imejitokeza kutokana na kuwepo kwa baadhi ya watu
wilayani Tunduru, kujenga dhana ya kuendelea kulaumu serikali kwamba,
imewasambazia vyandarua vyenye mayai ya kunguni na kusababisha kuwatesa hasa
nyakati za usiku wanapokuwa wamelala.
Nalicho alisema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa
kijiji cha Njenga wilayani humo, kwenye maadhimisho ya mkutano wa Malaria
Africa yaliyofanyika kiwilaya kijijini hapo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa, mbali na serikali kuwaokoa
wananchi wake wasiweze kushambuliwa na ugonjwa wa malaria, kwa kuwagawia
vyandarua vya msaada bado wamejitokeza kwenye vyombo vya habari wakilalamika
kwamba vina kunguni jambo ambalo sio la kweli, badala yake wanapaswa kuzingatia
usafi majumbani kwao hasa sehemu wanayolala.
Pamoja na mambo mengine aliwataka watendaji wa wilaya hiyo,
wakiwemo maafisa tarafa kupita vijijini kutoa elimu ya afya kwa wananchi wao, ili
kuweza kuondoa malalamiko mengine ambayo hayana msingi wowote.
No comments:
Post a Comment