Na Mwandishi wetu,
TUMEONA na tutazidi kuona wanaotangaza nia ya kuwania nyadhifa
mbalimbali, katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015 kuna
mengi yamejitokeza na bado yataendelea kujitokeza hivyo ni vyema tukayajadili
kwa mapana kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na hata nafasi ya urais.
Napenda kuhoji, je hao wanaotangaza nia wanatangaza nia kweli
au ni dhidi ya rushwa? kwa hali ya kawaida katika jamii yetu ya kitanzania
imegubikwa na wimbi la rushwa, hivyo msamiati huu umekuwa ni wa kawaida hivyo
hata mtu ukimtuhumu ni mlarushwa inaonekana ni jambo la kawaida.
Hivyo wengi wametegwa na rushwa, sitakosea nikisema mifumo
yetu imekuwa lege lege dhidi ya kupambana na vita ya rushwa tena hata ufisadi.
Wakati tukiyasemea haya hivi sasa tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, huko ndiko tunakotarajia
kuwapata viongozi watakao tuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, endapo
tutacheza karata nzuri nina hakika tutaweza kuwapata viongozi waadilifu na pia
endapo tutacheza vibaya tutaishia kupata viongozi ambao sio waadilifu hivyo
karata zetu, zitakuwa ni shida na mateso makubwa katika kipindi hicho cha miaka
mitano.
Wapo tulionamashaka nao, wapo tusiowajua na wapo tunaowajua
kwa undani na wenye uadilifu, hivyo bado tuna safari ndefu ya kuwapima na kuchukua
maamuzi sahihi na yenye kuweza kutuongoza.
Wapo waliofanya vizuri na waliofanya vibaya hivyo wote
tunawatambua, vilevile tunataka kuwaangusha walio waadilifu na pia wapo wanaotaka
kuwaangusha wasio waadilifu, katika hili nasema wote kwa sasa ni watangaza nia
tu.
Napata shida sana ninapoona, wanaotangaza nia kwa kuangalia
mienendo yao iwe ni wale waliokwisha onyesha uwezo wao au wanaotangaza nia ya kurithi
nafasi za udiwani, ubunge na hata urais?
Sijasikia kwa uwazi waliotangaza nia dhidi ya rushwa, ila
nasikia minong’ono ya rushwa tena kwa makundi ya wapambe yakiwa tayari kutumia
rasilimali watu na fedha, kuhakikisha tu yanafikia malengo yao waliyojiwekea.
Wapo waliojipanga kuwapigia chapuo wagombea wenye ukwasi na
wengine wamejipanga kuona viongozi waadilifu, wakipata nafasi ya kutuongoza
lakini vita kubwa dhidi ya rushwa sasa imekuwa butu kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwa pamoja na mifumo ya sheria na kitaasisi inayofanya kazi ya
kuidhibiti kuwa lege lege?
Je, kwa eneo ulilopo ni nani hasa ametangaza nia huku ajenda
yake ikiwa ni pamoja na vita dhidi ya rushwa na ufisadi?, ni mikakati gani
ameibuni ili kudhibiti rushwa na ufisadi?, Je ni wangapi wametangaza nia juu ya
kupambana na adui huyu?................ katika hili natambua majibu tunayo wenyewe.
Je, kwa namna gani
unamwona mgombea kama kielelezo cha vita dhidi ya ufisadi, ni sahihi kumpigia
kampeni mtu usiyemjua vizuri kwa sababu tu una maslahi yako binafsi?
Nyie wagombea mnao tutangazia nia hapa nchini katika kila mikoa na wilaya zake, mnaweza mkaweka wasifu wenu wazi hasa uadilifu katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi?
Ni mikakati gani mliyonayo mtakayoiweka ili kupambana na
rushwa na ufisadi? wapo wengine mna kashfa za ufisadi na rushwa je hamuoni nyie
ni kikwazo cha vita dhidi ya rushwa na ufisadi? je ni kitu gani mnatuambia
dhidi ya kashfa zinazowakabili?
Wapambe na wagombea ambako kila kukicha mnawaza kutoa rushwa
mnataka nini baada ya yule mnayempa “Saport” kupata uongozi, hivi kweli
atawajali wananchi waliompa kura kwa rushwa?
Je, hivi mnashindwa kujua tofauti iliyopo kati ya kiongozi
bora na bora kiongozi, Je, mnashinda kutwa nzima kutuaminisha sifa za mgombea
au wagombea wenu hamuoni huu ni unafiki
na usaliti dhidi ya taifa?
Umaskini umekithiri, huduma kwa jamii ni hafifu lakini bado
tunawaza kuwapigia chapuo viongozi wasio waadilifu, migogoro ndani ya jamii
inaibuka kila kukicha, chanzo chake ni kukosa uadilifu kwa viongozi wetu katika kuwaongoza wananchi.
Kadhalika nao uhasama unakua kila kukicha, rushwa na ufisadi
umechukua nafasi lakini bado tunawaza kuhonga
fedha na pombe kipindi cha uchaguzi, ili tuwachague wasio waadilifu na kuendelea kuitesa jamii, sitakosea nikisema yatupasa sasa tubadilike.
Hizi ni zama za uwazi na ukweli, haya yote mamlaka zilizopo zinayajua
lakini hazichukui hatua, ni nani sasa kati yetu achukue hatua, wengi
wananong’ona pale wanapohojiwa uadilifu wao.
Linapofika suala la uwajibikaji ni kiburi, utadhani ni haki yao
kupora mali ya umma wapo tayari hata kurubuni baadhi ya watu ilimradi tu wajisafishe ndani ya jamii, hivi kweli tunawapima viongozi wetu uadilifu wao
kabla hatujawachagua?
Ushauri wangu kama ndani ya kata yako au jimbo lako mliweza
kupata kiongozi mwadilifu ni vyema mkamchagua mwadilifu.
Pia kama mlimpata
mgombea asiye mwadilifu ni vyema mkatafuta aliyetangaza nia dhidi ya rushwa hakika
akisimama semeni, huyu ndiye mgombea pekee na atatufaa kuwa kiongozi imara
hivyo tusifanye makosa.
Hivi viongozi wa vyama vya siasa, wamejiandaa vipi kupambana
na changamoto hii ya rushwa ndani ya vyama vyao wakati wakuwapata wagombea? Je,
wamejipanga vipi kuwadhibiti wagombea watakaotoa rushwa?
Au wapo tayari kuona wagombea wao wakikaa katika nafasi za
uongozi, kwa jitihada yoyote ile hata kwa matumizi ya kugawa fedha chafu kila
kona? upi ni mustakabali wa wagombea wao na maslahi kwa taifa hili, endapo
wanatumia rushwa na hawadhibitiwi.
Pia katika hili tusifungwe na fikra mgando ambazo zimejengwa
kwa misingi ya itikadi za vyama vya siasa, dini, kabila, urafiki au uswahiba
maana huo ndio utakuwa mwanya wa rushwa na ufisadi ndani ya jamii pia utakuwa
ni kikwazo kikubwa, katika kumpata mgombea mwadilifu ndani ya chama na pia
kumpata kiongozi bora atakaye tuongoza kwa miaka mitano ijayo.
Hivyo katika harakati za kumpata kiongozi tusiende kwa hila
na chuki dhidi ya propaganda chafu, dhidi ya washindani wetu na pia uungwana
utumike pale tunapoona yupo anayeweza kutuongoza.
Ni vyema sasa tumpatie nafasi ili atuongoze kwa manufaa yetu
wote, kadhalika tuwakane wazi wazi wasiofaa, watoa rushwa na hata wapambe wao na
wachukuliwe hatua stahiki pale wanapobainika.
Pia tuwaepuke wagombea na wapambe kwa nafasi yoyote ile, kuanzia
ndani ya chama na hata nje ya chama ambaye dhahiri amejikita katika kununua
uongozi, ni imani yangu hafai na kamwe tutakuwa tumechagua chaguo lisilo sahihi
kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa letu, hivyo tujihadhari na watangaza nia wanaotumia
mwanya wa rushwa kupata madaraka, tuwatofautishe na tuwabaini sifa zao na
baadaye tuseme Yes or No.
Hitimisho langu ni kwamba, tukifeli katika mchakato huu kwa vigingi
vya rushwa, propaganda na siasa chafu tusitarajie kupata matokeo mazuri, hakuna
chema kitakachotokana na mfumo mchafu ili uzalishe matokeo mazuri hivyo tujihadhari
katika mchakato wa uchaguzi, na pia katika mchakato wa kuipata katiba mpya yatupasa tuzingatie hili.
No comments:
Post a Comment