Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
SERIKALI wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, imewaagiza
watendaji wote wa vijiji wilayani humo kuhakikisha kwamba wanasimamia na
kutekeleza ipasavyo sheria ndogo ndogo, ambazo zimetungwa na kupitishwa na
baraza la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya hiyo.
Aidha wameagizwa kuacha vitendo vya ulegevu, wakati
wanapotekeleza majukumu yao ya kazi na kusababisha mwanya kwa wananchi kuvunja
sheria husika, hatimaye maendeleo kushindwa kusonga mbele.
Katibu tawala wilayani Tunduru, Ghaibu Lingo alitoa agizo
hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Matemanga wilayani humo.
“Watendaji ambao mnajiona hamna uwezo wa kutekeleza majukumu
mliyopewa na serikali, ni muda muafaka sasa mkajiondoa wenyewe kwa kufuata
taratibu za kiutumishi ili muweze kuwapisha wengine, ambao wapo tayari
kulitumikia taifa hili”, alisema Lingo.
Alisema haiwezekani serikali iendelee kumfumbia macho mtendaji
ambaye hatekelezi majukumu yake ipasavyo, na kuiacha jamii ikivunja sheria na
taratibu zilizowekwa kwa makusudi au bila kujua hatimaye kusababisha hasara kwa
wananchi wengine.
No comments:
Post a Comment