Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Chande Nalicho akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo katika moja ya ziara yake ya kikazi ambazo amezifanya hivi karibuni. |
Na Steven
Augustino,
Tunduru.
CHANDE Nalicho ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,
amewataka wananchi wa vijiji vilivyopo katika tarafa ya Matemanga wilayani humo
kutumia nguvu zao na kujituma kwa hali na mali, kuhakikisha kwamba simba ambao
wamekuwa wakiwasumbua hasa nyakati za usiku wanauawa ili wananchi waondokane na
adha wanayoipata sasa ya kushindwa kuishi kwa amani.
Nalicho alitoa kauli hiyo, alipokuwa akikabidhi askari wa nane
idara ya wanyamapori wilayani humo, ambao walipelekwa katika tarafa hiyo kwa
lengo la kupambana na simba hao kuhakikisha kwamba wanauawa.
Hatua hiyo imefuatia kutokana na simba hao wamekuwa
wakishambulia mifugo ya wananchi hasa nyakati za usiku, jambo ambalo
linahatarisha hata usalama wa binadamu kwa wakazi wanaoishi katika vijiji vilivyopo
kwenye tarafa ya Matemanga.
Awali akitoa taarifa ya matukio hayo Mtendaji wa kata ya
Matemanga, Omary Hussein alieleza kuwa simba hao ambao walianza kuleta madhara
katika makazi ya watu mapema mwezi Februari mwaka huu, wamekwisha poteza uhai
wa mbuzi 25, mbwa 3 pamoja na kujeruhi ng’ombe 2.
Omary alifafanua kuwa pamoja na serikali kupeleka mara kwa
mara askari wanyama pori, lakini bado jitihada za kuwaua wanyama hao wakali
hazijazaa matunda na bado wananchi wa maeneo hayo, wanaendelea kuishi kwa hofu
kubwa.
Nao wananchi ambao walizungumza kwa nyakati tofauti walisema
kuwa mbali ya maelekezo ya viongozi kutolewa, yakiwataka wananchi kulala mapema
na kupunguza safari nyakati za usiku wamekuwa sasa wakilazimika kulala na
makopo makubwa ndani ya nyumba zao, ambayo huyatumia kujisaidia usiku kutokana
na kuogopa kwenda nje ya nyumba zao ambako wamejenga vyoo, wakihofia kutafunwa
na simba.
Akizungumza katika mkutano huo, Afisa ardhi na maliasili wa
wilaya ya Tunduru Japhet Mnyagala aliwahakikishia wananchi kuwa idara yake
itaendelea na msako mkali wa kuwaua wanyama hao wakali, mpaka pale tatizo hilo
litakapokuwa limekwisha.
Mnyagala alisema awamu hii askari wake, wamejiandaa na
wanarisasi za kutosha hivyo mafanikio ya kuwaua watashirikishwa wazee wa mila
ambao watawasaidia wakati wa kutekeleza zoezi hilo, kutengeneza na kutega hata
mitego ya asili ambayo inaweza kufanikisha kuwakamata kwa urahisi zaidi.
No comments:
Post a Comment