Na Kassian Nyandindi,
Namtumbo.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,
wametakiwa kutowaogopa watumishi na watendaji wa serikali waliopo katika wilaya
hiyo, badala yake wawabane na kuwahoji ikiwemo hata kufanya ufuatiliaji wa
fedha za miradi ya maendeleo ya wananchi, ambazo hupelekwa katika maeneo yao.
Mbali na hatua hiyo, pia wamehimizwa kuwashirikisha wananchi
ili nao waweze kushiriki vyema katika shughuli za miradi hiyo jambo
ambalo litawezesha wilaya, kufikia malengo yake iliyojiwekea ikiwemo kupiga
hatua katika nyanja ya kiuchumi.
Rai hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Stephen Nana
alipokuwa akizungumza na watumishi pamoja na madiwani katika kikao cha baraza
la madiwani, ambacho kiliketi mjini hapa.
Nana alisema ni lazima madiwani waache tabia ya kuwanyenyekea watumishi wa serikali, hata kama wanakabiliwa na hali ngumu ya kimaisha ambapo aliongeza kuwa woga wao utatoa nafasi kwa watumishi hao, kufanya kazi kwa mazoea na kusababisha hasara kwa taifa hili.
Kadhalika alieleza kuwa ufuatiliaji juu ya matumizi sahihi ya fedha za miradi ni jambo la lazima lisilo na mjadala, kwani kufanya hivyo kutasaidia fedha hizo kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa ikiwemo kuimarisha hata baadhi ya miundombinu na huduma za kijamii.
Alifafanua kuwa baadhi ya madiwani wa halmashauri ya Namtumbo
wamekuwa kikwazo kikubwa kwa kutotimiza majukumu yao ya kazi ipasavyo, kitendo
ambacho kinahatarisha kudorola kwa maendeleo ya wilaya hiyo na kusababisha
jamii kuendelea kuwa masikini.
“Hakuna pingamizi lolote kwa diwani kuhoji au kufuatilia matumizi ya fedha za maendeleo zinazoletwa na serikali kwa ajili ya mradi fulani katika kata au wilaya, isipokuwa ni lazima ufuatiliaji ufanyike kikamilifu kwenda katika eneo la mradi ili kuweza kubaini ubora wa mradi husika, mkifanya hivyo mtafanya utekelezaji wake uwe katika viwango”, alisema Nana.
No comments:
Post a Comment