Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
PENDEKEZO la kuligawa Jimbo la Mbinga Mashariki, lililopo
wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma limeingia dosari kufuatia kuwepo kwa malalamiko
yanayodaiwa kwamba mchakato huo wa kuligawa jimbo hilo, umefanywa na viongozi
wachache bila kushirikisha wadau mbalimbali wa wilaya hiyo, kitendo ambacho
kimeelezwa kuwa ni ukiukwaji wa maagizo na taratibu zilizotolewa na tume ya
taifa ya uchaguzi hapa nchini.
Baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo, walitoa malalamiko hayo walipokuwa
wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti huku wakiitaka
serikali kuwa makini na suala hilo ambalo kutokana na wadau husika kutoshirikishwa
kama vile taratibu za tume katika kurekebisha mipaka, kugawa majimbo na
kubadili majina zinavyotaka.
Mapendekezo hayo ya kuligawa jimbo hilo yamefanyika muda wa
nusu saa katika kikao cha dharula cha baraza la madiwani, kilichoketi Mei 27
mwaka huu kwenye ukumbi wa Jumba la maendeleo mjini hapa.
Hata baadhi ya Madiwani ambao walikuwepo katika kikao hicho
nao walionesha kushangazwa na hali hiyo, wakisema kuwa walitumiwa ujumbe kwa
njia ya simu kwamba wanatakiwa katika kikao cha dharula kwa tarehe hiyo, bila
kufafanuliwa kinahusu nini na walipowasili walikutana na ajenda hiyo ya pendekezo
la kuligawa jimbo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa takwimu za
wilaya ya Mbinga kwa mujibu wa sensa ya idadi ya watu na makazi iliyofanyika
mwaka 2012 wilaya hiyo inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 385,354 idadi ambayo
haitoshelezi katika kufanya mgawanyo wa watu kwa majimbo mawili.
Vigezo na taratibu zilizotolewa na tume ya uchaguzi Mei 10
mwaka huu, ambazo nakala yake tunayo inaagiza kuwa vitatumika katika kuchunguza
mipaka na kugawa majimbo kwa uchaguzi wa wabunge, huku mgawanyo wa wastani wa
idadi ya watu (Population quota) unapaswa kuzingatiwa.
Jimbo la Mbinga mashariki ambalo kwa sasa limetolewa
pendekezo la kuligawa majimbo mawili, la Mbinga mjini lenye idadi ya watu
129,537 na vijijini kuna watu 255,817 idadi ambayo imefafanuliwa kuwa ni ya
watu wachache katika kufanya mgawanyo wa majimbo hayo.
Kadhalika mkazi mmoja wa kata ya Matarawe Mbinga mjini, Hamis
Nanyanje akizungumzia hilo alisema kuwa mchakato huo wa kuligawa jimbo la
Mbinga Mashariki kuwa majimbo mawili kwa sasa ni mapema mno, sawa na kuitwisha
serikali mzigo mzito pasipo sababu ya msingi kwa kile alichodai kuwa kutokana
na kuwepo kwa idadi ndogo ya watu, katika wilaya hiyo.
Naye Astery Ndunguru alifafanua kwamba
itakuwa ni jambo la kushangaza endapo mgawanyo huo serikali itaridhia huku
akitolea mfano, hata kwa Manispaa ya Songea ambayo idadi yake ya watu ni kubwa
hawana majimbo mawili, hivyo alihoji inawezekanaje kwa wilaya ya Mbinga ambayo
idadi yake ya watu ni ndogo igawanywe kuwa na majimbo mawili ya uchaguzi ?.
“Majimbo ya uchaguzi yanayostahili
kuwasilisha maombi kwa mujibu wa utaratibu ulioainishwa na tume ni yale yenye
idadi kubwa ya watu wasiopungua 325,000 kwa majimbo ya mjini na watu 235,000
kwa majimbo ya vijijini”, alisema Ndunguru.
Cosmas Haulle mkazi wa kata ya Maguu
alibainisha kuwa katika mgawanyo huo tume ya uchaguzi imekuwa ikizingatia pia
suala la upatikanaji duni wa mawasiliano katika eneo husika kama vile barabara,
simu, redio na magazeti vimekuwa vikipewa kipaumbele ambapo kwa wilaya hiyo
mawasiliano hayo yamekuwa yakipatikana kwa urahisi kuliko kwenye maeneo mengine.
Hata hivyo alipohojiwa Mkurugenzi
mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Hussein Ngaga juu ya malalamiko
hayo ya wadau mbalimbali kutoshirikishwa katika kikao hicho cha mapendekezo ya
mgawanyo huo wa majimbo alisema; “mimi nipo safarini sijui huo mchakato huko
umeendeleaje, hayo malalamiko ambayo wadau wamekuletea naomba uyapuuze, huenda
walipewa taarifa kwa njia ya barua wao hawakufika na haiwezekani sisi tushindwe
kupitisha mchakato huu kwa sababu suala hili lilikuwa na uharaka”, alisema Ngaga.
No comments:
Post a Comment