Saturday, May 30, 2015

KANISA KUMFIKISHA MAHAKAMANI DIWANI

Askofu mkuu wa jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, John Ndimbo.
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

UONGOZI wa Kanisa katoliki Jimbo la Mbinga mkoani Ruvuma, umesema upo katika hatua za kumfikisha Mahakamani Diwani wa kata ya Litembo kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Mbinga mkoani humo, Altho Hyera kwa kile walichodai kuwa diwani huyo amekuwa akitishia usalama wa wafanyakazi wa hospitali ya Litembo na kuharibu kwa makusudi, sifa ya hospitali na maendeleo yake.

Hospitali hiyo ambayo humilikiwa na jimbo hilo, umeeleza pia diwani huyo amekuwa akimdhalilisha Askofu mkuu wa jimbo la Mbinga, John Ndimbo kwa kuandikia barua kwa viongozi wa juu wa serikali ambazo gazeti hili nakala zake imezipata zikimtuhumu Askofu huyo kuwa ni mla rushwa, ameshindwa kusimamia maendeleo husika na ameitelekeza hospitali hiyo.

Taarifa ya uongozi wa kanisa katoliki wilayani humo, kutaka kumfikisha kizimbani kiongozi huyo wa CCM zilielezwa katika kikao kilichowakutanisha baadhi ya waumini wa vigango vya kanisa hilo kata ya Litembo, ambao ulifanyika kwenye ukumbi wa Parokia ya Litembo uliopo katika kata hiyo.


Askofu Ndimbo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, alisema kuwa amesikitishwa na mwenendo na tabia zinazofanywa na kiongozi huyo wa kisiasa ambapo amechukua jukumu la kuitisha mkutano huo, baada ya kuona anachafuliwa pasipo sababu yoyote ile kwa kuandikiwa barua ambazo zinalenga kuharibu mahusiano kati yake, kanisa na viongozi wa serikali.

“Ndugu zangu waumini napenda niwataarifu kwamba, tuhuma zote ambazo diwani huyu ameziandika katika barua zake ni za uzushi na zenye kujenga hila, jukumu tulilochukua tukiwa kama kanisa tumezifikisha kwenye vyombo vya usalama (Polisi) kwa hatua zaidi na taratibu zitakapokamilika, hatua husika zitachukuliwa dhidi yake,

“Leo inafikia hatua mimi naambiwa mla rushwa na nimeitelekeza hospitali hii, kweli jamani tunakwenda wapi, siku zote hayati Mwalimu Julius Nyerere katika uhai wake alikuwa akisema, mtu mwenye akili timamu hawezi kuukataa ukweli imenisikitisha sana”, alisema Ndimbo.

Alifafanua kuwa hata katika kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Mbinga, tuhuma hizo amezifikisha kupitia Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo, Senyi Ngaga kwa hatua zaidi.

Kwa upande wake akizungumza katika kikao hicho Afisa tawala wa hospitali ya Litembo, Padri Raphael Ndunguru alisema kuwa sasa imefika hatua wamechoshwa kuharibiwa sifa ya uongozi wa hospitali na utawala wa jimbo kwa ujumla, kwa mambo ambayo hayana ukweli.

“Ndugu zangu tunatoa rushwa kwa Askofu kwa faida gani, mambo haya aliyoyaandika ni ya uzushi tu na ameiingizia serikali yetu hasara kubwa, kila alipokuwa akiandika kwa viongozi wa juu tume mbalimbali zimewasili hapa kwetu kuja kuchunguza na kubaini hakuna ukweli wowote, kwa nakala hizi za barua ambazo zinaendelea kutuchafua sisi tunasema imetosha tunauwezo wa kumfikisha mahakamani”, alisema Padri Ndunguru.

Padri Ndunguru aliongeza kuwa kutokana na hali hiyo, imefikia hatua sasa mshikamano uliokuwepo awali kati ya waumini wao na kanisa hivi sasa unapungua hivyo hawaoni sababu ya kuendelea kukalia kimya jambo hili, badala yake hatua stahiki zitachukuliwa ili kuweza kudhibiti yasiweze kuendelea.

Alisema kuwa tuhuma hizo zimekuwa zikipandikizwa kisiasa, jambo ambalo linasababisha ustawi wa maendeleo hospitali ya Litembo kuanza kurudi nyuma kutokana na Hyera kupandikiza chuki na majungu, pasipo sababu yoyote ile msingi.

Kadhalika alibainisha kuwa uongozi wa jimbo la Mbinga unamshangaa diwani huyo kuingilia mambo ya kanisa kuchanganya na siasa, wakati wao wamekuwa wakilenga maendeleo katika kutoa huduma ya kimwili na kiroho kwa waumini wao.

“Ningependa kuwaasa ndugu zangu tuwe na akili timamu na za juu ili tuweze kufikiri vizuri juu ya masuala ya kimaendeleo na kuacha kujenga malumbano yasiyokuwa ya lazima, kujengeana hila kama hizi ambazo hazina faida kwetu hazitufikishi mbali katika mipango ya kimaendeleo, kila kitu ndugu zangu juu ya maendeleo kinategemea sana kiongozi aliyebora tunahitaji mtu aliyekuwa na mawazo ya juu”, alisema.

Padri Ndunguru alieleza kuwa hospitali ya Litembo ambayo huendeshwa na jimbo katoliki la Mbinga, hivi sasa ina miaka 22 tokea kuanzishwa kwake hapakuwa na matatizo yoyote kama hayo na kwamba hawataendelea kufumbia macho hali hiyo.  


Hata hivyo kwa upande wake alipoulizwa na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, Diwani wa kata hiyo Altho Hyera alisema yeye huletewa malalamiko na wafanyakazi wa Hospitali hiyo na yeye huyafanyia kazi.

No comments: