Sunday, May 10, 2015

WANANCHI TUNDURU WAISHI KWA HOFU SIMBA WALETA BALAA

Na Steven Augustino,
Tunduru.

WANANCHI waishio katika vijiji ambavyo vipo kata ya Matemanga, Ndenyende, Milonde, Fundimbanga na Namwinyu katika tarafa ya Matemanga wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wanaishi katika hofu ya kuvamiwa na kutafunwa na mnyama mkali aitwaye Simba.

Hofu hiyo imetokana na kundi la wanyama hao, kuvamia katika maeneo hayo na kuanza kuleta madhara ya kuua mifugo ya wananchi.

Taarifa kutoka katika maeneo hayo zinafafanua kwamba, tayari wameua na kula mbuzi 18 na mbwa wa nne mali ya baadhi ya wakazi wa maeneo hayo.

Wananchi hao walisema, simba hao ambao wamekuwa wakionekana kuzunguka mara kwa mara walianza kuwasumbua mwishoni mwa mwezi Machi, mwaka huu hali ambayo inaendelea kuwaweka kwenye wakati mgumu na kuwafanya waishi kwa wasiwasi.


Khadija Kalola na Sekemani Kaesa walisema kwa nyakati tofauti kuwa kuwepo kwa taarifa za wanyama hao, kunathibitishwa kuwa nyao zao ambazo usiku wanapolala na kuamka asubuhi huzikuta wamekanyaga wakitembea kuzunguka nje ya nyumba zao.

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wananchi zinaonesha kwamba simba hao, kati yao wanaonekana kuwa ni wazee, wamehama katika hifadhi ya taifa ya Selou baada ya kushindwa mapambano ya kuwinda.

Akizungumza kwa niaba ya askari wa idara ya wanyama pori, Charles Shawa alisema hivi sasa wameongeza nguvu wakiendelea kuwasaka pamoja na kuandaa mitego ili waweze kuwanasa.

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho amewataka wananchi kuwa na subira wakati serikali ikiendelea kuwasaka wanyama hao na kuwaua, ili wasiendelee kuleta madhara.

Nalicho aliwaasa wananchi hao waachane na safari za kutembea usiku, hasa katika kipindi hiki cha msako mkali, ambacho serikali inapambana na simba hao.


No comments: