Na
Steven Augustino,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, imeagiza na
kuwataka wakulima wa korosho wilayani humo kuanza palizi mapema katika mashamba
yao ya mikorosho, ili kuweza kuboresha zao hilo na kuzalishwa kwa wingi.
Faridu Khamis, ambaye ni Mwenyekiti wa halmshauri hiyo alitoa
agizo hilo kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi hivi karibuni,
ukumbi wa Klasta ya walimu mlingoti mjini hapa.
Khamis alisisitiza kuwa wakati wakulima hao, watakapokuwa
wanafanya palizi katika mashamba yao waache vitendo vya uchomaji moto ambapo
wakifanya hivyo, wanaweza wakasababisha mikorosho kuungua.
Alifafanua kwamba, hamasa hiyo anaitoa kufuatia kuwepo kwa taarifa
kuwa wakulima wa zao hilo katika wilaya yake wamekwisha tengewa mgao wa tani
302,270 za madawa aina ya Sulpher duts, ambayo yatatumika kupulizia mikorosho
yao.
Mgao huo utatolewa kutoka katika mfuko wa Wakfu, ambao unafanya
kazi ya kuendeleza zao la korosho Tanzania (CIDTF) ambapo mpaka sasa umeweza
kutenga lita 6,392 za madawa mbalimbali ya maji kwa ajili ya kupulizia zao
hilo.
Awali akitolea taarifa ya ujio wa madawa hayo Mwenyekiti wa mfuko
huo, Athuman Nkinde alieleza kuwa madawa hayo yatafikishwa kwa wakulima husika
wilayani humo mwishoni mwa mwezi huu.
Nkinde alisema madawa yote yatafikishwa katika ofisi za vyama vya
ushirika wilayani Tunduru, na kwamba yatauzwa kwa bei husika ya ruzuku ambayo
imepangwa na mfuko.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, mfuko mmoja wa Sulpher duts ambao
una ujazo wa kilo 25 utauzwa kwa shilingi 15,000 badala ya 45,000 ambayo huuzwa
na walanguzi, kitendo ambacho humuumiza mkulima na kumfanya aendelee kuwa
maskini.
Alisema lengo la mfuko kuweka bei hiyo ni kumkomboa mkulima huyo
mwenye kipato cha chini, na kwamba mgao wa pembejeo hutolewa kwa kuzingatia
uzalishaji wa korosho ambapo katika msimu wa mwaka 2014/2015 wilaya hiyo,
ilipewa mgao wa kilo 7,452,339.
No comments:
Post a Comment