Na Kassian
Nyandindi,
Mbinga.
BAADHI ya wazee na vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata
ya Mbinga mjini mkoani Ruvuma, wamemtaka Diwani wa kata hiyo Kelvin Mapunda kwenda
kuchukua fomu muda utakapofika kwa ajili ya kugombea tena, nafasi ya udiwani katika
kata hiyo.
Aidha walieleza kuwa wapo tayari kutoa fedha zao mfukoni kwa
ajili ya kumchangia fomu ya kuwania nafasi hiyo, kwa kile walichoeleza kuwa
wamejenga imani naye kutokana na kazi zake alizozifanya katika kipindi cha
miaka kumi ya uongozi wake aliowaongoza.
Wazee na vijana hao walisema hayo walipokuwa wakizungumza na
mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti mjini hapa, huku wakiongeza kuwa
wao wanaona ndiye mwanachama ambaye yupo karibu nao katika kuendeleza maendeleo
yao kwa faida ya sasa, na kizazi kijacho.
“Tokea aingie madarakani mwaka 2005 hadi sasa, tunaona ndiye
kiongozi ambaye anapaswa kuendelea kutuongoza katika kata hii amekuwa akishirikiana
na wananchi kwa mambo mbalimbali ya kijamii, hivyo hatuna budi kumpatia nafasi
aendelee kutuongoza”, walisema.
Waliendelea kueleza kuwa ushirikiano aliokuwa nao,
wamependezwa hasa katika kupigania ujenzi wa barabara za lami na kituo cha
kisasa magari ya abiria Mbinga mjini, kuboresha elimu, afya na mambo mengine ya
kimaendeleo jambo ambalo linamfanya ang’are kuliko wengine.
Mapunda alipoulizwa na mtandao huu kama yupo tayari kugombea
tena katika nafasi hiyo, alithibitisha kupokea maombi ya wazee na vijana wa
CCM, huku akifafanua kwamba atatekeleza hilo pale muda utakapowadia.
“Ndugu yangu kwa sasa siwezi kuzungumza sana juu ya hili,
lakini tuombe Mungu pale muda utakapowadia naweza nikazungumzia suala la kuendelea
kuwaongoza wananchi wangu katika kata hii ya Mbinga mjini au la, wengi
wamenifuata na kunitaka niendelee”, alisema Mapunda.
Pamoja na mambo mengine, serikali hapa nchini katika mpango wake
wa kusogeza huduma karibu na wananchi, imeweza pia kuongeza kata katika mji wa
Mbinga na kufikia kata nane ambazo ni Mbinga mjini A na B, Matarawe, Mbambi,
Luhuwiko, Betlehemu, Masumuni na Lusonga ambazo kufikia uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, watachaguliwa madiwani watakaoweza
kuongoza kata hizo.
No comments:
Post a Comment