Na Muhidin
Amri,
Songea.
MPANGO wa kunusuru kaya maskini ulioratibiwa na mfuko wa
maendeleo ya jamii nchini (TASAF) awamu ya tatu, Manispaa ya Songea mkoani
Ruvuma umeweza kuibua kaya maskini 8492 sawa na asilimia 106 ikiwa ni ongezeko
la kaya 464 ambazo zilikadiriwa hapo awali kufikiwa na mpango huo, katika Manispaa
hiyo.
Aidha hadi sasa TASAF imeweza kutekeleza kazi zake katika
mitaa 53 ya mjini hapa, ambayo nayo iliingizwa kwenye mpango kwa lengo la kukabiliana
na changamoto zilizopo, hatimaye kuweza kufikia malengo iliyojiwekea.
Mratibu wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika Manispaa ya
Songea, Christopher Ngonyani alieleza hayo, alipokuwa akizungumza na mwandishi
wetu ofisini kwake.
Ngonyani alidai kuwa uhaulishaji wa miradi ya mfuko huo,
katika baadhi ya maeneo unakwamishwa na wanasiasa ambao huwadanganya wananchi
wasishiriki katika utekelezaji wake, jambo ambalo aliongeza kuwa linahatarisha
kurudisha nyuma jitihada zinazofanywa na serikali katika kupunguza umaskini na
ajira kwa wananchi.
Mbali na hayo, kumekuwa pia na tatizo kwa baadhi ya kaya
ambazo ziliandikishwa kwenye mpango huo wa TASAF kwa ajili ya kufanyiwa
utekelezaji, baadhi yao wamekuwa wakihama makazi yao kutoka sehemu moja kwenda
nyingine kitendo ambacho husababisha kukosekana kwa mlengwa, ambaye aliandikishwa
katika eneo lake na kufanya akose huduma husika.
Pia Mratibu huyo anaiomba jamii kuachana na maneno ya
wanasiasa ambao wanaonesha kutokuwa na nia njema kwao, badala yake washiriki
kikamilifu ili kuweza kunusuru kaya ambazo huishi katika mazingira hatarishi
ili kutimiza adhima ya serikali, kuwafikia walengwa wote waliopo kwenye mpango
huo.
Kadhalika amewataka kujenga tabia ya kuhudhuria mara kwa mara
katika shughuli zote ambazo zimepangwa na TASAF, ikiwemo kufanya ufuatiliaji wa
tarehe za malipo ya fedha zao na kujihusisha kwenye kazi sambamba na kuchangia
nguvu zao ili miradi iliyopangwa, iweze kufikia malengo na kukamilika kwa
wakati uliopangwa.
No comments:
Post a Comment