Na Julius
Konala,
Songea.
MAOFISA ugani katika Halmashauri nne zilizopo mkoani Ruvuma,
wameweza kujengewa uwezo juu ya matumizi sahihi, katika tekinolojia mpya ya
uhifadhi wa mazao.
Lengo la maofisa hao kupewa elimu hiyo, ni kuwataka katika
maeneo ambayo wanafanyia kazi mkoani humo, waende kwa wakulima vijijini
wakawaelimisha juu ya tekinolojia hiyo na baadaye waweze kuhifadhi mazao yao
katika hali nzuri.
Mafunzo juu ya matumizi sahihi ya uhifadhi wa mazao,
yalifanyika jana kwenye ukumbi wa mikutano Walimu SACCOS mjini Songea, ambayo
yalikuwa yakiendeshwa na shirika la CARITAS na CRS.
Jumla ya maofisa ugani 32 kutoka wilaya ya Songea, Namtumbo, Mbinga
na Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameweza kupata elimu hiyo.
Mwakilishi mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Georgina Mbawala alisema
washiriki hao mara baada ya kumaliza kupewa mafunzo hayo watakuwa walimu
wazuri, katika suala la uhifadhi huo ambao unalenga kuhifadhi mazao katika
kipindi cha miaka mitatu bila ya kushambuliwa na wadudu waharibifu.
Naye Ofisa mradi kutoka katika shirika hilo PICS CARITAS jimbo
kuu la Songea, Brito Mgaye amewataka wakulima kutumia tekinolojia hiyo
watayopewa na maofisa hao wa ugani, ili kupunguza upotevu wa mazao yao mara
baada ya mavuno shambani pamoja na kuwapunguzia gharama ya ununuzi wa madawa ya
kilimo ambayo hutumika kupulizia wakati wa kuhifadhi mazao katika maghala.
Alisema kuwa asilimia 50 ya mazao ya wakulima hupotea kwa
kushambuliwa na wadudu waharibifu, kutokana na wengi wao kutokuwa na
tekinolojia ya kisasa juu ya uhifadhi wa mazao yao.
Wakuu wa wilaya na wakurugenzi mkoani Ruvuma, wameshauriwa kuipokea
tekinolojia hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa wakulima itawaondolea adha kubwa
katika kuhifadhi mazao yao, na kuwafanya waweze kukuza uchumi wao.
No comments:
Post a Comment